Raia nchi 71 ruksa kuingia Tanzania bila viza

DODOMA; RAIA wa nchi 71 hawahitaji viza wanapoingia Tanzania, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula ametoa kauli hiyo bungeni leo Juni 4, 2025 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk Pius Chaya aliyetaka kujua ni jitihada gani zimefanyika kurahisisha upatikanaji wa viza kwa watalii wenye uraia tofaui wanaokuja nchini kwa mwitikio wa Royal Tour.

“Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imeanzisha mfumo wa maombi ya viza kwa njia ya mtandao (e-Visa) unaowawezesha watalii kuomba viza popote walipo duniani bila kulazimika kufika ubalozini.

“Halikadhalika, Serikali imeboresha Kanuni za Uhamiaji za mwaka 2023 (GN 428) ambapo kwa sasa watalii wanaotumia Visitors Pass wanaruhusiwa kutembelea Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kurejea Tanzania bila hitaji la kuomba upya pasi ya kuingia nchini alimradi pasi aliyopewa iwe haijaisha muda wake.

“Serikali imeendelea kuingia makubaliano na nchi mbalimbali ili kurahisisha utaratibu wa viza, ambapo kwa sasa raia wa nchi 71 hawahitaji viza wanapoingia nchini.

“Aidha, kwa sasa watalii kutoka mataifa mengi zaidi duniani wanaruhusiwa kupata viza wanapowasili (visa on arrival) kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa kama Julius Nyerere (Dar es Salaam), Kilimanjaro na Zanzibar,” amesema Naibu Waziri.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button