Raia wa Ureno ahukumiwa kwa kuishi nchini kinyemela

RAIA wa Ureno, George Ferreira amehukumiwa kulipa faini ya Sh 500,000 au kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuwapo nchini kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Amri Msumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo, Msumi alisema ingawa mshitakiwa aliingia nchini kwa njia halali lakini kuendelea kwake kuishi nchini baada ya viza yake kuisha muda haibadilishi ukweli kwamba ni mkosaji.
Alisema baada ya mshitakiwa kukamilisha adhabu yake afanye utaratibu wa kurasimisha uwapo wake au arudishwe nchini kwao.
Katika utetezi wake, George alikiri viza yake na pasipoti kuisha muda wake na kwamba, alishindwa kurudi nchini Ufaransa ambako ndio makazi yake, kwa ajili ya kufanya mchakato wa hati mpya ya kusafiria pamoja na viza kutokana na janga la Covid-19. Alisema pia yupo katika mpango wa kuomba uraia wa Tanzania.
Awali mahakamani hapo, wakili wa serikali, Hadija Masoud alidai kuwa Machi 6 mwaka huu katika eneo la Fire, Wilaya ya Ilala ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa raia wa Ureno mwenye hati ya kusafiria namba P 087318 alikutwa akiwa anaishi nchini kinyume cha sheria baada ya viza yake kuisha muda.
Aliieleza mahakama kuwa tarehe hiyohiyo mshitakiwa alifikishwa katika ofisi ya uhamiaji Kurasini ambapo alihojiwa kwa njia ya onyo baada ya kutajiwa haki zake za msingi na katika mahojiano alikiri kuwa viza na paspoti yake imeisha muda wake.



