Rais Mwinyi avunja ukimya waziri kujiuzulu

ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amevunja ukimya kujiuzulu kwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Simai Mohamed Said na kumtaka kusema ukweli.

Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Februari Mosi, 2024 na kusema kuwa Waziri akitaka kujiuzulu kuna utaratibu wake na sio kukurupuka kwenda kwenye vyombo vya habari na kutangaza kujiuzulu.

“ilipotokea ajali ya mabomu kule gongo la mboto, mimi nikiwa Waziri wa ulinzi nilipeleka ujumbe kwa Rais wangu wakati huo Mhe.Kikwete nikimtaka aliridhie nijiuzulu lakini sikukurupuka kwenda kwenye vyombo vya habari nikatangaza kwamba nimejiuzulu sio utaratibu,”amesema Rais Mwinyi na kuongeza

Advertisement

“Utaratibu unataka umwambie aliyekuteua akubali ndio ukatangaze kujiuzulu, Mhe.Kikwete akasema hii ni ajali huna sababu ya kujiuzulu, hakuna mtu aliyesikia kama nilitaka kujiuzulu leo nasema hili hadharani lakini sikuwahi kulisema kabla.

Aidha, Rais Mwinyi amesema kuwa Waziri anapojiuzulu ni vema akasema ukweli kilichosababisha kujiuzulu ili umma ufahamu.

“Kama tumezuia kitu na wewe una biashara hiyo tangaza, sema ukweli, sema ukweli hapa kuna mgongano wa kimaslahi mimi ni muagizaji wa kitu fulani na ninyi mmezuia, lazima tuwe wa kweli sasa hivi ukitoka halafu ukaenda kuwaaminisha watu kinyume chake si sahihi, ” amesema Rais Mwinyi

Amesema amekuwa akifuatilia mitandao ya kijamii na kuona watu wakidai kuwa Zanzibar hajawahi kujiuzulu mtu, si kweli, wakati wa ajali ya meli kuna Waziri alijiuzulu na alijiuzulu si kwasababu alisababisha yeye ile ajali kawajibika kwasababu ni sekta anayoisimamia na kilichotokea ilikuwa ni uzembe na si ajali.

“Suala la kujiuzulu waziri ni suala ambalo si geni ni moja katika njia ya kuwajibika, katika wizara kunaweza kukawa na mazingira mawili ya waziri kujiuzulu.

Mazingira ya kwanza yanaweza kuwa katika sekta yako inayoisimamia kumetokea tatizo au changamoto na wewe kama Waziri unawajibika kwa changamoto ile, si lazima uwe umeifanya wewe lakini unawajibika kwasababu wewe ndio msimamizi wa sekta.

“Sababu nyingine ya waziri kujiuzulu ni pale ambapo serikali inaamua jambo na wewe ukubaliani nalo, unatoka unajiuzulu kwasababu hukubaliani na maamuzi yaliyotolewa na serikali lakini kuna jambo moja lazima tukumbushane wakati unawajibika kwa njia yeyote ile ya kwanza au ya pili ni lazima uwe mkweli na ukweli naozungumzia hapa ni kama kuna mgongano wa maslahi utangaze.

“Uwaziri sio nafasi ambayo utakaa nayo maisha kuna njia nyingi ambazo zitakutoa kwenye uwaziri, aidha utaondolewa au utawajibika kwa tatizo litakalotokea, unapochukua sekta hizi ujue kuna matatizo ambayo yanaweza kutokea na matatizo hayo wala si lazima usababishe wewe na pale ambapo hukubaliani na serikali sema na kuwa muwazi tutakuheshimu zaidi, kama una baa watu wamezuia pombe sema mimi nina baa inaingilia na maslahi yangu, kuwa muwazi,”amesisitiza Rais Mwinyi.

Kauli ya Mwinyi imekuja ikiwa ni siku sita tangu aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Simai Mohamed Said kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai mazingira si mazuri ya kazi.