Rais kutuma ujumbe polisi leo

Rais kutuma ujumbe polisi leo

RAIS Samia Suluhu Hassan Jumanne anatarajiwa kuzungumza na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi mkoani Kilimanjaro.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime amesema Rais Samia atafungua kikao kazi cha maofisa wakuu waandamizi wa makao makuu, makamanda wa polisi mikoa na vikosi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Misime alisema Jeshi la Polisi kila mwaka hufanya kikao kama hicho kufanya tathmini ya utendaji kwa kipindi cha mwaka ili kuona wapi walifanya vizuri na wapi hawakufanya vizuri na sababu zake na kuweka mikakati kuongeza ufanisi kwa mwaka unaofuata.

Advertisement

Rais Samia anazungumza na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi zikiwa zimepita wiki kadhaa tangu aseme anataka mabadiliko na ufanisi katika jeshi hilo.

Alisema hayo katika Ikulu Dodoma wakati akiwaapisha viongozi aliowateua akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura.

“Tutakwenda kutizamana huko upatikanaji wa watendakazi ukoje kwa majeshi yote, yote yote, tutakwenda kutizamana vizuri kama yalishapita lakini huko mbele tunapokwenda tutachujana vizuri, ili kujenga majeshi yenye sifa na hadhi ya kuisimamia nchi hii,” alisema Rais Samia.

Ameunda timu ya watu 12 ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Chande, Makamu Mwenyekiti, Balozi Mstaafu Ombeni Sefue na sekretarieti ya watu watano itakayomshauri na kumpa mapendekezo ya maoni na hatua za kuchukua.

“Nimeunda ili inishauri kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wenye matokeo chanya bora kwenye vyombo vyetu vyote vya haki jinai na tukimalizia polisi tutakwenda majeshi mengine hadi tumalize,” alisema Rais Samia.

Alisema serikali inakuja na jicho jingine katika kuyasuka majeshi yake na kusisitiza kuwa watasimamia kila jeshi linapomalizwa kuchunguzwa na tume hiyo linafanyiwa maboresho na kuja na miundo inayofaa na bora zaidi.

Awali Rais Samia aliiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi wafanye mageuzi ya kiutendaji na uadilifu ndani ya jeshi hilo ili kulijengea imani kwa wananchi.

Alitoa maagizo hayo wakati akifunga mafunzo ya kozi ya uofisa wa polisi Na.1/2021 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini Dar es Salaam.