Rais Museveni wa Uganda kufanya ziara Tanzania
RAIS wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, anatarajiwa kuwasili nchini kesho Februari 07, 2026 kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Dar es Salaam imesema katika ziara hiyo, Rais Museveni atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
SOMA: Tanzania, Uganda zasaini makubaliano kuinua sekta ya mafuta na gesi
Mazungumzo yao yatajikita kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, na kujadili masuala muhimu ya kikanda na kimataifa.
Miongoni mwa masuala yatakayozungumzwa ni suala la nishati, hususan Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), ambao unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa nchi zote mbili na kanda kwa ujumla.
Rais Museveni na Rais Samia pia watazungumza na vyombo vya habari kuhusu mazungumzo yao.
Ziara hiyo inakuja wakati ambapo nchi zote mbili zinaendelea kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara, usalama, na miundombinu.
Rais Museveni anatarajiwa kuondoka nchini baada ya kumalizika kwa ziara hiyo.



