Rais Samia achangia 100m/- Harambee ya CCM

DAR ES SALAAM — Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amechangia Sh milioni 100 katika harambee ya kitaifa ya chama hicho iliyofanyika leo Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Harambee hiyo inalenga kukusanya Sh bilioni 100 kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na ujenzi wa Makao Makuu mapya ya chama.
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi, alisema hafla hiyo imeshirikisha wanachama na marafiki wa chama kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku akisisitiza kuwa fedha zitakazopatikana zitasaidia kufanikisha maandalizi ya uchaguzi na miradi mikubwa ya maendeleo ya chama.
Katika harambee hiyo, wageni mashuhuri walioketi meza kuu walichangia jumla ya Sh milioni 270, wakiwemo Dk. Philip Mpango (Sh milioni 20), Dk. Hussein Mwinyi (Sh milioni 50), Kassim Majaliwa (Sh milioni 20), Hemedi Suleiman Abdallah (Sh milioni 20), Stephen Wasira (Sh milioni 20), Dk. Tulia Ackson (Sh milioni 20) na Zuber Ally Maulid (Sh milioni 20).
CCM upande wa Zanzibar ilichangia Sh bilioni 4 na kuahidi Sh bilioni 1 zaidi. Kampuni ya GSM, kupitia Rais wa Klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said, ilitoa Sh bilioni 10, huku Klabu ya Yanga ikiahidi Sh milioni 100.
Pia, Mtume Boniface Mwamposa alichangia Sh milioni 50 kwa ajili ya kampeni na ujenzi wa makao makuu mapya ya chama.