Rais Samia afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri

DAR ES SALAAM – Rais Samia Suluhu Hassan, ametangaza mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri, sambamba na uteuzi muhimu katika nyadhifa mbalimbali serikalini. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, mabadiliko hayo yanalenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi serikalini.

Katika mabadiliko hayo, Prof. Palamagamba Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, huku William Lukuvi sasa atakuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu. 

Jenista Mhagama ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Afya, akitoka katika nafasi yake ya awali katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, Balozi Pindi Chana ameteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii akichukua nafasi ya Angellah Jasmine Kairuki, ambaye ametajwa kuwa Mshauri wa Rais.

SOMA: Mpango shule salama kwa maendeleo ya wanafunzi

Aidha, Hamza Johari ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akitokea kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA). 

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Pia Bw. Samwel Maneno ameteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiwa amewahi kuwa Mshauri wa Kisheria wa Rais. Anachukua nafasi ya Balozi Prof. Kennedy Gastorn, ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Sheria na Mikataba. 

Vilevile Rais Samia amemteua Dk Ally Saleh Possi kuwa Wakili Mkuu wa serikali. Kabla ya uteuzi huo Dk Possi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi.

Taarifa ya Ikulu imesema viongozi hao wataapishwa kesho Agosti 15 katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Habari Zifananazo

Back to top button