Rais Samia aipaisha korosho Afrika

DAR ES SALAAM – RAIS Samia Suluhu Hassan amesema amekubaliana na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi waunde umoja wa wazalishaji wa zao la korosho ili kuwa na sauti moja katika masoko ya korosho duniani.

Aidha, amesema wamekubaliana na Rais Nyusi kuimarisha biashara na uwekezaji baada ya kubaini zimepungua kwa kiwango kikubwa.

Soma:http://Samia: Mazao ya korosho, ufuta na mbaazi yanalipa

Rais Samia alisema hayo wakati yeye na mgeni wake, Rais Nyusi walipozungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam.

Rais Nyusi leo anafungua Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF)maarufu Sabasaba yanayofanyika katika Viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa.

Akizungumzia kuimarisha ushirikiano kwenye kilimo, Rais Samia alisema Msumbiji na Tanzania ni wazalishaji wa korosholakini si wapangaji wa bei ya zao hilo katika soko la dunia.

“Tunajitahidi kupanga bei ya ndani. Tumekubaliana kuunda umoja na mnakumbuka alipokuja Rais Embalo wa Guinea -Bissau nilimuuzia wazo hili na amekubali, tutashirikiana ili wazalishaji wa korosho Afrika tuwe na sauti kwenye masoko ya korosho,” alisema Rais Samia.

Rais Nyusi amesema wamekubaliana kufanya kazi pamoja kuzalisha zaidi korosho na kuhakikisha zao hilo
linawanufaisha wazalishaji.

“Tunachokiona sasa korosho zinachukuliwa na wenzetu wa nje na sisi hatunufaiki ipasavyo, hivyo ni lazima tufanye utafiti kuona zao hili itakavyokuwa na nguvu ya pamoja kwa wazalishaji wa korosho Afrika,” amnesema.

Juni 21 mwaka huu Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Embalo aliwasili nchini kwa ziara ya siku tatu na katika mazungumzo yake Juni 22 mwaka huu Ikulu -Dar es Salaam na Rais Samia walizungumza kuhusu ushirikiano
katika zao la korosho.

Guinea -Bissau inazalisha zao hilo kwa wingi na kuuza nchini India na asilimia 10 ya pato la nchi hiyo hutokana
na zao la korosho lakini asilimia 80 ya wakulima wa zao hilo ni wadogo.

Biashara na Msumbiji Rais Samia alisema kwa sasa hali ya biashara na Msumbiji imeshuka ikilinganishwa na miaka ya nyuma hivyo wameliona hilo.

Alitoa mfano wa takwimu za mwaka jana zinaoonesha Tanzania ilifanya biashara na Msumbiji ya Dola za Marekani milioni takribani 17 wakati mwaka uliotangulia kiwango kilikuwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 57.

 

Habari Zifananazo

Back to top button