Rais Samia amesikia kilio maaofisa usafirishaji – Mpogolo

DAR ES SALAAM: SERIKALI imepunguza gharama za leseni kwa maofisa usafirisha wa bodaboda, bajaji na guta zinazotumia umeme katika bajeti ya mwaka 2025-2026 kulipia kiasi cha Sh 30,000.
Hatua hiyo imedhihirisha usikivu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wake hususani maofisa usafirishaji.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa madereva guta za umeme yaliyofanyika katika chuo cha Polisi ikiwa ni mwezi mmoja toka atangaze maofisa hao wanahakikisha wanasajiliwa.
Akizungumza na madereva hao, wakufunzi na viongozi wa shirikisho la maafisa hao Mpogolo amesema usikivu wa Rais Samia umeendelea kuhakikisha vilio vya madereva wa vyombo vya moto vinasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani.
Ameeleza kuwa kutolewa kwa mafunzo hayo na jeshi la polisi kutasaidia kuongeza uelewa na usalama, kutambulika rasmi kama familia kwa kusajiliwa tofauti na awali hawakuwa na leseni na hawakujulikana kwa urahisi.
SOMA ZAIDI
Katika mafunzo hayo, Mpogolo, amebainisha kuendelea kutoa ushirikiano kwa vijana walionufaika na mafunzo hayo kutoka maeneo mbalimbali kufanya shughuli zao vizuri katikati ya jiji kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu watazowekewa ili kupunguza msongamano katika masoko.
Amesisitiza madereva wa maguta ya umeme, kufuata na kusimama katika sheria za barabarani kutokana na mafunzo waliyopata ili wanufaike kiuchumi kwa kujali muda wao na watumiaji wengine wa barabara.
Mpogolo, ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha vijana kutumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi, ili waweze kusaidia familia zao na kutoa mchango wa maendeleo kwa serikali, kwa kuwa kazi ni msingi wa utu.
“Na tayari jeshi la polisi limewafundisha misingi ya kazi yao , Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewasajili na kutambulika rasmi katika sekta ya usafirishaji, na Mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini (LATRA) imewapa leseni ili wafanye kazi kwa amani wakiwa barabarani,” amesema Mpogolo.
Akizungumzia juu ya nishati safi Mpogolo amesema Rais Samia ni kinara namba moja wa kusisitiza matumizi ya nishati hiyo ni vema madereva wa maguta ya umeme kutumia vizuri fursa hiyo kwa kufanya kazi kwa uaminifu, usalama wa dereva, chombo chake, na kuwa na mahusiano mema kwani dunia ya sasa inafanya kazi kwa mtandao na wateja wanataka mizigo ifike haraka kwa kutumia usafiri ambao unatumia umeme.
Aidha,Mpogolo ametoa shukrani kwa jeshi la polisi, wakiongozwa na Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania IGP Camillus Wambura, kwa kukubali ombi la kufanyika kwa mafunzo ya madereva maguta ya umeme kwa kupunguza gharama za masomo toka laki moja hadi elfu arobaini, na Mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini (LATRA) kwa kutoa leseni.
Kwa upande wao madereva maguta, katika risala yao wameomba serikali iwasaidia kuangalia na kupunguza bei ya betri za maguta, maguta na maeneo ya maegesho mjini.
Ombi ambalo, Mpogolo amelipokea na kuahidi kulifanyia kazi kwa kuhakikisha Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Dar es salaam Elihuruma Mabelya atawapangia na wahakikishe wanafuata sheria, utaratibu na wasizibe njia na atatekaidi achukuliwe hatua.
Huku akiwasisitiza kujiunga katika vikundi vya Saccos ya shirikisho, kujisajili na kuomba mikopo ili waweze kupata mafanikio ya kazi zao kutokana na mikataba kandamizi.
Pamoja na kushughulikia suala la vipuri serikali itazungumza na kampuni zinazotengeneza maguta ya umeme waje kuwekeza nchini hali itayosaidia kuondoa madalali wa kati wanaoongeza bei za vifaa na kudhibiti upandishwaji wa bei.
Mafunzo hayo yamefungwa kwa wahitimu wote kupatiwa vyeti, leseni na kuahidi kufuata sheria za usalama barabarani huku wakiwataka vijana wengine kwenda kupata mafunzo jambo litalosaidia kupunguza changamoto za kazi ya usafirishaji mizigo na vifurushi kwa haraka.
Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni mwezi mmoja tangu Mpogolo na Mabelya kukutana na madereva hao katika viwanja vya mnazi mmoja na kuwataka kusajiliwa ili watambulike rasmi.