Rais Samia apuliza kipenga Katiba mpya

RAIS wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Mutungi, kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa lengo likiwa ni kuwashirikisha wadau katika kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu kuhusu demokrasia ya Vyama vingi vya siasa nchini.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Rais Ikulu, Zuhura Yunus imeeleza kuwa Rais Samia ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kilichofanyika Ikulu ya Chamwino na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali kuhusu kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kikao hicho kimejadili namna ya kushirikisha wadau mbalimbali na hasa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato huo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Mbali na mchakato wa Katiba mpya, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi, zikiwemo Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Aidha, miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Jenista Mhagama, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro na Watendaji wa Taasisi mbalimbali.

Habari Zifananazo

Back to top button