Rais Samia asisitiza SADC kumaliza migororo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

MWENYEKITI wa asasi ya siasa, ulinzi na usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amezisisitiza nchi za Jumuiya hiyo kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kumaliza uhasama uliopo baina ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC na Rwanda chini ya mchakato wa Angola.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema hayo kwa niaba ya Rais Dk. Samia alipomwakilisha kufungua Mkutano wa Viongozi Wakuu na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika leo Novemba 20 katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.

Advertisement

SOMA: Dk Mwinyi kumwakilisha Rais Samia mkutano SADC

Rais Dk. Samia amefafanua kuwa wakati nchi za SADC zikiendelea kujadili hali ya Usalama wa Mashariki ya DRC ni vyema kukawekwa mifumo imara ya Ufuatiliaji na utekelezaji wa maazimio yanayoidhinishwa na Jumuiya mbalimbali za Kikanda ikiwemo yale ya Umoja wa Afrika(AU) na Umoja wa Mataifa (UN).

Ameeleza kuwa hatua hiyo itawezesha kupatikana kwa misaada ya kifedha na kilojistiki kwa wakati na kuongeza Ufanisi wa Misheni za SADC na kupunguza gharama.

Rais Dk. Samia amezishauri nchi za SADC kutumia majadiliano ya Mkutano huo kutoka na maazimio yatakayokuwa chachu ya kupatikana kwa amani ya kudumu katika Ukanda wa SADC na kuwa ni ushahidi wa dhamira ya nchi hizo ya kuleta amani endelevu.