Rais Samia awafuta kazi Makamba, Nape

DODOMA – Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Utenguzi wa Waziri wa Habari umekuja siku chache baada ya wachambuzi wa siasa na watetezi wa demokrasia kumnyoshea kidole Nape Nnauye kufuatia kauli ya “utani” aliyoitoa wakati wa ziara huko Bukoba mkoani Kagera.

Wakati sababu za kumuondoa January Makamba katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje hazijafahamika, Rais Samia amemteua Balozi wa Tanzania nchini Italia, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje.

Advertisement

Katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka Rais Samia amemteua Jerry Silaa kuwa Waziri wa Habari, Mawasialiano na Teknolojia ya Habari. Silaa alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nafasi hiyo itaongozwa na Deogratius John Ndejembi aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema, Rais amemteua Ridhiwani Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). 

Pia Rais Samia amemteua Cosato David Chumi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye atapangiwa kituo cha kazi.

Vilevile Taarifa hiyo imesema Deus Clement Sangu ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Huku Dennis Lazaro Londo akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Makamba, Stephen Lujwahuka Byabato ameondolewa katika nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine Rais Samia amemteua Eliakim Chacha Maswi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria. Kabla ya uteuzi huu Bw. Maswi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA);

Bi. Mary Gaspar Makondo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma. Kabla ya uteuzi huu Bi. Makondo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria. Bi. Makondo anachukua nafasi ya Bi. Rehema Sefu Madenge ambaye amestaafu;

Wengine walioteuliwa ni Bw. Kiseo Yusuph Nzowa ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro. Kabla ya uteuzi huu Bw. Nzowa alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu;

Bw. Musa Haji Ali ameteuliwa kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi huu Bw. Ali alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu;

SOMA: ‘Dira ya Taifa ya Maendeleo ni picha, maono’

Bw. Louis Peter Bura ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato. Bw. Bura anachukua nafasi ya Bw. Said Juma Nkumba ambaye amepangiwa majukumu mengine;

Bi. Kemirembe Rose Lwota amehamishwa kutoka Wilaya ya Manyoni kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti;

Dk. Vincent Biyegela Mashinji amehamishwa kutoka Wilaya ya Serengeti kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya Manyoni;

Dk. Maulid Suleiman Madeni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti;

Bw. Afraha Nassoro Hassan amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Bw. Hassan anachukua nafasi ya Bw. William Anyitike Mwakalambile ambaye uteuzi wake umetenguliwa; na

Bw. Dennis Kwame Simba ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). Kabla ya uteuzi huu Bw. Simba alikuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

 

/* */