Rais Samia; Chombo cha utulivu, uwazi na somo la demokrasia Tanzania

RAIS Samia Suluhu Hassan amefungua nafasi za kisiasa na uhuru wa kujieleza.
Baada ya kuingia madarakani alifuta marufuku ya mikutano ya kisiasa iliyokuwa imewekwa kabla ya utawala wake ulioanza Machi 21, 2021. Hatua hii iliruhusu vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara, jambo lililokuwa haliruhusiwi kwa miaka sita.
Aidha, Rais Samia amewezesha kufunguliwa baadhi ya vyombo vya habari vilivyofungiwa. Serikali chini ya Rais Samia iliruhusu baadhi ya magazeti na redio zilizofungiwa wakati wa utawala uliopita kurejea ‘hewani.’ Aidha, aliwezesha mchakato wa mazungumzo na wadau wa habari.
Kimsingi, Rais Samia ameonesha utayari mkubwa kukutana na wanahabari na kujadili changamoto za sekta hiyo, jambo ambalo awali lilikuwa nadra kutokea. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya ‘Mama Samia’ imeruhusu ukosoaji na kutoa mwito kwa wadau kuwa na ukosoaji chanya kwa serikali.
Ukosoaji chanya huonesha mafanikio, upungufu na kupendekeza njia za kufanya jambo kuwa bora zaidi. Mara kadha Rais Samia ametoa kauli kadhaa zinazohamasisha watu kutoa maoni yao kwa heshima. Mfano, mara kadhaa alitoa kauli na kusisitiza kuwa ukosoaji wa serikali si uadui na hili ni sawa na darasa la demokrasia.
Ameanzisha Kamati ya Mapitio ya Demokrasia
Katika juhudi za kuimarisha demokrasia, Rais Samia alianzisha Kamati ya Mapitio ya Demokrasia inayojumuisha wawakilishi kutoka vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari. Kamati hiyo ilikusanya maoni na mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kisiasa na utawala nchini.
Mapendekezo ya kamati hii yalijumuisha kurekebisha sheria za uchaguzi, kuimarisha iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuongeza uwakilishi wa wanawake na makundi maalumu katika siasa. Machi 8, 2023 katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyopfanyika Moshi,
Rais Samia alitangaza kwamba serikali itaunda kamati maalumu kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya na demokrasia yenye usawa. Katika maadhimisho hayo Rais Samia anasema: “Muda si mrefu tutatangaza kamati
ambayo itashughulikia jambo hilo.”
Si hayo tu, Rais Samia pia amewezesha kuondolewa vikwazo vya kisiasa kwani mwaka Machi 2023, serikali yake iliondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani, hatua iliyotumika kama sehemu ya uhuisho wa mazingira rafiki ya kisiasa nchini.
Kupitia tume ya wadau na ripoti Oktoba 21, 2022, Rais Samia alipokea ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa mwaka 2022. Kikosi hicho kilikuwa na jukumu la kukusanya mapendekezo kutoka kwa wadau juu ya demokrasia na vyama vingi na kuwasilisha ripoti hiyo iliyolenga utekelezaji wa haraka wa marekebisho kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.
Kupitia baraza la vyama vya siasa Septemba 11, 2023, ‘Serikali ya Mama Samia’ ilifungua rasmi mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau zaidi ya 700 kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi na hali ya siasa.
Marekebisho ya sheria za uchaguzi, Tume ya Uchaguzi
Serikali ya Rais Samia ilipitisha muswada wa sheria unaolenga kuimarisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kufanya mchakato wa uchaguzi kuwa huru na haki. Muswada huu unalenga kuondoa uteuzi wa makamishna wa uchaguzi kutoka kwa Rais badala yake, ufanywe na jopo huru linalojumuisha majaji.
Aidha, Rais Samia amewezesha mapitio ya sheria kama lilivyokubaliwa na Bunge, Februari 2024. Sheria hizo mpya zinaongeza uwazi katika uteuzi wa wakurugenzi na maofisa wa tume kwa kutoa nafasi kwa jopo kuhakiki na kuteua, badala ya uteuzi wa moja kwa moja kutoka kwa halmashauri za mkoa. Hii ni hatua kuelekea uchaguzi huru na wa haki zaidi Oktoba 2025.
Samia amekukuza uwakilishi wa wanawake na makundi maalumu
Rais Samia ameonesha dhamira ya kuimarisha usawa wa kijinsia na uwakilishi wa makundi maalumu katika
siasa. Alihamasisha vyama vya siasa kuongeza idadi ya wanawake na vijana katika nafasi za uongozi.
Aidha, aliongeza idadi ya wanawake katika Baraza la Mawaziri na katika nafasi za uongozi serikalini, hatua inayothibitisha dhamira yake ya kukuza usawa wa kijinsia.
Haya yanaoneshwa wazi juhudi za Rais Samia kuimarisha uwakilishi wa wanawake na makundi maalumu; chini ya uongozi wa Mama Samia, mawaziri wanawake wameongezeka kutoka 5 hadi 7 katika mabadiliko ya baraza la mawaziri ikiwa ni pamoja na Waziri wa Ulinzi, Stergomena Tax kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.
Katika uongozi wake, Rais Samia amethibitisha kuwa wanawake wameshika vyeo vya juu. Mfano, Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Afya na uwakilishi katika ngazi za wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala wa mikoa na wilaya mbalimbali.
Mikakati ya usawa wa kijinsia, vijana na watu wenye ulemavu
Kupitia ripoti nyingi za Machi 2025, Rais Samia amehamasisha haki za wasichana kupata ardhi, bima ya afya ya wote na haki ya kisheria. Rais Samia amesisitiza usawa wa kijinsia kuwa haki ya kikatiba, si zawadi na kuwaonesha vijana umuhimu wa uwajibikaji wa kijamii.
Mpango mmoja wapo wa mfano ni Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kusaidia watu wengi wakiwamo wanawake waliokumbana na ukatili na kuboresha usiri wa kisheria.
Aidha, Rais Samia amewezesha uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake. Alianzisha na kukuza Mradi wa Maendeleo ya Ujasriamali kwa Wanawake (WEDP) kwa msaada wa Benki ya Dunia na kuwezesha wanawake wengi kupata mikopo nafuu na mafunzo.
Afungua nafasi kwa upinzani na kuimarisha haki za binadamu
Rais Samia alikubali kurudi kwa viongozi wa upinzani waliokuwa uhamishoni, akiwamo Tundu Lissu. Aidha, alianzisha mchakato wa maridhiano na vyama vya upinzani. Aliwezesha mchakato wa mazungumzo ya kisiasa na kuanzisha kikosi kazi kusimamia mageuzi ya kisiasa ikiwa ni pamoja na rasimu ya katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na haki za mwelekeo usio wa CCM.
Mama huyu ni chombo cha utulivu, uwazi na somo la demokrasia Tanzania pia amekutana mara kadhaa na viongozi wa upinzani kujadili siasa za nchi. Kwa mara ya kwanza, alihudhuria tukio la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Siku ya Wanawake mwaka 2022 na kuonesha matumaini ya kujenga uhusiano bora zaidi na wapinzani.
Aidha, alikemea mauaji ya kisiasa na kuagiza uchunguzi kufanyika. Rais amewezesha na ametia nguvu katika demokrasia ya Tanzania kwa kuhakikisha uwazi, uwakilishi na uwajibikaji katika mfumo wa kisiasa. Kupitia Falsafa yake ya ‘4R’, Rais Samia ameweka msingi wa kuleta ufanisi, uwajibikaji na amani.
Ujasiri wake wa kuleta suluhisho la kisiasa na uwajibikaji, umekuwa sababu kubwa ya kupata sifa kubwa na pongezi kitaifa na kimataifa hakika ‘Mama Samia’ anastahili sifa kubwa maana amekuwa chombo cha utulivu, uwazi na somo la demokrasia nchini Tanzania na sasa Tanzania ina nyota mpya ya uongozi uliojikita katika haki,
maendeleo na dira ya kisiasa kwa wote.



