Rais Samia Suluhu Hassan kesho septemba anatarajiwa kuzindua jengo la kisasa la ghorofa la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) lililopo barabara ya Arusha-Moshi kata ya Sekei jijini Arusha.
Hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella na kuwataka wananchi wa Arusha na viunga vyake kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais kwani anakuja kufanya jambo la kihistoria katika Mkoa wa Arusha.
Mongella alisema kuwa Rais anatarajiwa kuwasili Arusha leo na kupokelwa na viongozi mbalimbali wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA kabla ya kwenda Ikulu ndogo ya Arusha kwa mapumziko.
Alisema serikali imejipambanua kikubwa katika kuleta mageuzi makubwa ya kidijitali hivyo uzinduzi wa jengo la PAPU ni matokeo tosha ya jinsi gani huduma ya Posta inataka kutoka ilipo ili isonge mbele zaidi katika kutoa huduma kibiashara.
RC Mongela alisema kuwa kwa sasa Posta imejipanga kutaka kutoa huduma kisasa na kwa wakati kwa wateja wake ili kuondoaka na zana za kufanya kazi kizamani.
‘’Serikali imejipanga kuleta mageuzi makubwa ya kidigital lengo ni kutaka kusukuma uchumi wa Nchi na kuboresha shirika la Posta kutaka kufanya kazi kisasa zaidi’’alisema Mongella
Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo alisema kuwa shirika hilo limejipanga kikamilifu kwa kuwa vitendea kazi vyenye uhakika katika shughuli zao za kila siku na kuondokana na kufanya kazi kizamani kama awali.
Alisema Posta sio ile ya zamani kwani ya sasa imejipambanua Kidigital na kutaka kufanya kazi kisasa zaidi ili kwenda na wakati kwani dunia ya sasa iko kiganjani hivyo watendaji wanapaswa kwenda na kasi ya shirika hilo.
Postamasta alimshukuru Rais kwa kuliboresha shirika hilo kwani kwa sasa lina zana na vitendea kazi vya kisasa lengo ni kutaka kutoa huduma bora na sio bora huduma.
Awali wiki mbili zilizopita Kamati nne za Baraza la Utawala la PAPU zilikutana Arusha lengo lilikuwa kujadili kwa kina bajeti na sera hususani katika kujikita kidigital na kuondokana katika kufanya kazi kizamani na kufanya kazi kisasa na kibiashara haswaa.
Kamati hizo ilishauri watendaji wa PAPU kuwa teknolojia inavyokuwa kwa kasi ni wakati wa Mashirika ya Posta Afrika kufanya kazi kisasa ili wateja wa mashirika hayo waweze kufurahia huduma za mashirika ya hayo ya Posta Afrika tofauti na ilivyokuwa zamani.