Rais wa Shirikisho la Soka Colombia akamatwa

Rais wa Shrikisho la Mpira wa Miguu Colombia, Ramón Jesurún.

RAIS wa Shrikisho la Mpira wa Miguu Colombia(FCF), Ramón Jesurún, na mtoto wake wamekamatwa baada ya kutokea ugomvi wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini’Copa América‘ Julai 14 katika jiji la Miami, Marekani.

Ramón, 71, na Ramón Jamil, 43, wamekamatwa kwa tuhuma za kumshambulia afisa usalama katika eneo hilo, imesema Idara ya Polisi ya Miami-Dade.

Tuhuma hizo zinahusiana na ugomvi kwenye uwanja wa Hard Rock baada ya Colombia kupoteza kwa Argentina kwa bao 1-0 katika muda wa nyongeza. Sio Ramón wala mtoto wake aliyetoa maelezo rasmi kuhusu tikio hilo.

Advertisement

Katika taarifa ya Idara ya Polisi ya Miami-Dade tukio hilo limetokea baada tu ya mchezo kumalizika ambapo Argentina imetwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Ramón na mwanae walikuwa “wakitembea kuelekea lango la uwanja, lakini walikasirika na kuanza kumfokea mmoja wa maafisa wa usalama, ambaye alikuwa ameagizwa na uongozi wake kuzuia watu kwa muda wasiende eneo hilo,”imesema taarifa.

Polisi wamesema afisa usalama huyo aliweka kiganja cha mkono wake kifuani mwa mtoto wa Ramón ili kumrudisha nyuma jambo lililomkasirisha baba yake.

Soma: Argentina yaanza vyema kutetea taji la Copa America

Kisha Ramón alimsukuma afisa huyo huku mwanae akimkaba shingo afisa usalama huyo na kumvuta hadi chini akimpiga ngumi na teke kichwani.

“Mtoto wa Ramón pia alimkamata na kumsukuma afisa wa kike aliyejaribu kusaidia,” Polisi wamesema.

Taarifa hiyo ya polisi imesema watuhumiwa hao pia walimpiga ngumi meneja wa usalama.

Ramón, mtoto wake na watu wengine wa familia hiyo wanaamnika walikuwa wakijaribu kuingia uwanjani kushiriki utoaji tuzo baada ya mchezo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Colombia halijatoa kauli mara moja kuhusu suala hilo.

Mchezo huo wa fainali ulichelewa kuanza kwa dakika 80 baada ya mashabiki wasiokuwa na tiketi kulazimisha kuingia kwenye uwanja wa Hard Rock.

Watu kadhaa wamekamatwa baada ya kukabiliana na polisi na maafisa usalama huku wengine kadhaa wakipatiwa matibabu.