UBELGIJI : RAIS wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amewataka washirika wake wa Ulaya kuendelea kushikamana katika msaada wao kwa Ukraine, hasa linapokuja suala la usalama wa taifa hilo, badala ya kugawanyika.
Zelensky aliyasema hayo wakati wa mkutano muhimu uliofanyika katika makazi rasmi ya Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte. SOMA: Mawasiri NATO kukutana Brussels
Mkutano huo ulikusudiwa kujadili mustakabali wa Ukraine, ikiwa ni pamoja na hali ya usalama, hasa katika muktadha wa kutarajiwa kurejea kwa Donald Trump madarakani.
Kiongozi wa Ukraine alizungumzia pia kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, jambo ambalo linaendelea kuwa changamoto kubwa.
Katika mkutano huo, Rais Zelensky alikutana na viongozi wakuu wa Ulaya, akiwemo Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy, na Rais wa Poland, Andrzej Duda. Lengo la mkutano lilikuwa ni kujadili hatua za mbele kuhusu usalama wa Ukraine na mustakabali wake katika janga la vita na Urusi.