MKUU wa Mkoa Kagera, Hajjat Mwassa amewataka wakazi wa mkoa kuwa watulivu, kuzingatia taratibu uchaguzi na kurejea nyumbani badaa ya kupiga kura huku wakisubiri matokeo.
Akizungumza mara badaa ya zoezi hilo kukamilika kwenye Kituo cha Uwanja wa Ndege mtaa wa Pwani kata ya Miembeni leo Novemba 27, RC Mwassa ameonya yoyote atakayejaribu kuanzisha vurugu atachukuliwa hatua.
“Mkoa wa Kagera unasifika kwa ustarabu, utulivu,busara na hekima hatuwezi kukubali wala kuruhusu zoezi la uchaguzi litugombanishe kila kitu kitakuwa salama,”amesema Mwassa.
Katika zoezi hilo RC Mwassa aliambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Nkwera na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Siima katika Manispaa ya Bukoba.
Aidha viongozi hao wametembelea vituo mbalimbali ikiwemo kituo cha Kilima Hewa, Katatwolansi, Kashai Halisi, Miembeni, Kahororo na sehemu nyingine ambazo uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaendelea.
Mwassa amewahakikishia wananchi wa Mkoa Wa Kagera usalama na amani na kuwaomba kila mmoja kuzingatia usalama wake bila kuathiri usalama wa mtu mwingine.
“Ninachofurahia ni kuwa katika vituo vyote mwitikio wa wananchi imekuwa mkubwa sana hii inayoonyesha kuwa huenda tutamaliza mapema sana katika Manispaa ya Bukoba nimefurahishwa na wananchi walivyokitokeza ,naomba kama mtu yuko nyumbani aje kupiga kura mara moja kwa ajili ya mabadiliko ya mtaaa na jamii kwa ujumla, “amesema.
Mkoa wa Kagera unatarajiwa kuwa na zaidi ya wapiga kura milioni 1.5 na vituo vya wapiga kura 4,012.