RC Kagera ataka mabadiliko ya kilimo mwaka 2023

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amedhamiria kuanza mwaka 2023 kwa kuhakikisha wakazi wa Kagera wanainuka kiuchumi kupitia kilimo cha mazao ya ndizi na kahawa pamoja na mazao mengine ambayo yanaonekana kustawi kwa wingi mkoani humo.

Chalamila amesema serikali imeona mafanikio katika zao la kahawa,  ambalo limeonekana  kuleta kipato kikubwa kwa wananchi,  baada ya wakulima kupata miche bora bure au kwa gharama ndogo tofauti na mazao mengine, ambayo hata upatikanaji wa mbegu umekuwa changamoto sana.

Alisema miaka ya nyuma Mkoa wa Kagera ulikuwa unazalisha ndizi kwa wingi, lakini kwa sasa inaonekana zao la ndizi linaendelea kupoteza mwelekeo na uzalishaji unaendelea kuwa wa kawaida kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo magonjwa yanayoshambulia migomba kama mnyauko.

“Kama kiongozi wa Mkoa wa Kagera, nimekuwa nikipokea malalamiko mbalimbali, hasa watu wengi utasikia mkoa huu ni masikini, lakini ukiangalia hata masuala ya uzalishaji wa ndizi, ambalo ndilo zao la biashara unakuwa sio mzuri sana, mwaka 2023 ni wa mabadiliko makubwa, nataka kushirikiana na wadau kuhakikisha tunarudisha zao la ndizi kama namba moja mkoani Kagera,”alisema Chalamila.

Alisema mikakati ya uboreshaji wa ndizi unaenda sambamba na upatikanaji wa migomba kwa bei nafuu, kuboresha huduma za ugani, uboreshaji wa huduma za utafiti katika chuo cha kilimo cha Maruku, kutafuta masoko, pamoja na kuhakikisha wataalamu wa kilimo wanaenda kujifunza mbinu mpya za uzalishaji  wa zao la ndizi katika nchi zinazofanya vizuri.

Aliyataja mazao mengine ambayo yanatarajiwa kupewa kipaumbele na kufanya vizuri kwa mwaka 2023 kuwa ni kila kaya wakazi ya mkoa wa Kagera  kupanda miche 10 ya parachichi shambani, kurejesha zao la vanilla, kulima alzeti kwa wingi pamoja na kutafuta uwekezaji katika mashamba ya chai.

Hata hivyo alisema ili kufanya mipango hiyo kufanikiwa ni kuhakikisha wadau ambao wako ndani na nje ya nchi kuhakikisha wanafanya uwekezaji wa kujenga viwanda vya kuongeza thamani katika mazao mbalimbali, ili kuhakikisha soko linakuwepo mwaka mzima.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button