TANGA; Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba, amewataka wananchi mkoani humo kuacha tabia ya kutembea na kiasi kikubwa cha fedha, badala yake watumie mifumo ya kadi za kibenki kufanya miamala mbalimbali.
Hayo amesema leo wakati wa uzinduzi wa msimu mpya wa kampeni ya Mastabata Halipoi, inayofanywa na benki ya NMB mkoani humo.
Amesema kuwa katika karne hii ya maendeleo ya kiteknolojia hakuna umuhimu wa kutembea na kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali, ili kujiepusha na majanga ikiwemo uporaji.
“Jengeni utaratibu wa kuhifadhi fedha benki na kupitia hii kampeni ya mastabata ndio imekuja kutupa umuhimu wa kutumia mifumo ya kadi katika kufanya miamala kwa njia salama zaidi,”amesema RC Kindamba.
Ofisa Mkuu wa wateja binafsi na biashara wa benki ya NMB, Filbert Mponzi amesema kuwa kampeni hiyo imelenga kuzawadia wateja wao wanaotumia NMB Mastercard au lipa mkononi (QR) fedha taslimu pamoja na zawadi nyingine ikiwemo safari kutalii.