MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema ili Mkoa huo uweze kukua kiuchumi katika sekta mbalimbali zikiwemo za ulishaji vyakula ni lazima kuwepo kwa miundombinu bora ya barabara ili kuvutia wawekezaji wengi.
Malima amesema hayo wakati wa kikao cha 40 cha bodi ya barabara cha Mkoa huo kilichofanyika Oktoba 5,2023 mjini Morogoro.
Amesema ili kukuza uchumi wa Morogoro na kuvutia wawekezaji, suala la uboreshaji wa miundombinu ya barabara haliepukiki.
Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi wa Mkoa huo kushirikiana kwenye kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo ya barabara.
“Kwa sasa hali ya barabara katika Mkoa wetu hairidhishi ,hivyo ni wajibu kwa mameneja wetu wa Mkoa wa Wakala ya Barabara Tanzania na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini kushirikisha viongozi katika utekelezaji wa miundombinu hii muhimu katika uchumi wa Mkoa” amesema Malima
Mkuu wa Mkoa pia amewaomba Wabunge wa Mkoa huo kuunga mkono Mipango mkakati ya vipaumbele na kuchochea ukuaji wa Maendeleo ya Kiuchumi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya Tarura kwa asilimia zaidi ya 300 na kutaka watendaji kusimamia vyema matumizi na kuteua wakandarasi wenye uwezo na sifa za kufanya kazi za miradi ya barabara Vijijini na mijini ikiwemo ya Tanroads.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro ,Mhandisi Lazeck Kyamba akiwasilisha taarifa amesema Mkoa huo umeidhinishiwa zaidi ya Sh bilioni 24 katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Mhandisi Kyamba amesema kati ya fedha hizo sh bilioni tatu zimeidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutoka Mfuko wa Maendeleo, na kiasi cha sh bilioni 20 zimeidhinishwa kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja .