Takukuru kuchunguza kampuni zinazodaiwa AMCOS Geita

GEITA: SERIKALI imeiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia kampuni zote ambazo zimeshindwa kulipa madeni ya Vyama vya Msingi vya Kilimo na Masoko (AMCOS) mkoani Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ametoa maagizo hayo kupitia kwa Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba alipomwakilisha katika Jukwaa Kuu la Vyama vya Ushirika mkoani humo.

Komba amesema taarifa zinaonyesha kuwa wapo wakulima wa zao la pamba na tumbaku, katika wilaya za Bukombe, Mbogwe na Chato, ambao wanazidai kampuni za ununuzi fedha zaidi ya sh milioni 218.
Amesema ili kusimamia haki ya mkulima inapatikana madeni hayo yatafuatiliwa na kamati za usalama za wilaya chini ya uratibu wa Takukuru kusaidia kudhibiti mianya ya dhuluma kwa wakulima.
“Jambo hili lisiwe la ushirika pekee yake, tulibebe sote kwa pamoja, wenzetu wa Takukuru na vyama vya Ushirika tuwaite haya makampuni yanayodaiwa.

“Makampuni haya yaitwe mbele ya kamati za ulinzi na usalama waeleze kwa nini wanakaa na fedha hizi za wakulima kwa muda mrefu”, amesema Komba na kuongeza;
“Kama tunavyosema nyinyi mlipe madeni, nasi tutashirikiana nanyi kukusanya madeni, ili kwa pamoja tuunusuru ushirika kwenye maeneoe yetu” amesema.
Aidha amewasihi viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia haki za wadau wote wa ushirika ambao ni wakulima, wanunuzi, halmashauri na ushirika wenyewe ili kumaliza changamoto za madeni.

“Kwa mjibu wa taarifa halmashauri zetu zinadai takribani sh milioni 52, wanunuzi wanadai takribani sh milioni 168 wadau hawa wasipolipwa stahiki zao tunahatarisha uhakika wa soko”, amesema.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, Dk Elfas Msenya amesema vyama vya ushirika mkoani Geita vina jumla ya wanachama 5,084 kutoka katika Vyama Vikuu Vitatu vya Ushirika.
Ametaja vyama vikuu ni Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe, (MBCU) Chama Kikuu cha Ushirika Geita (GCU) na Chama Kikuu cha Ushirika Chato (CCU) vinavyohudumia jumla ya AMCOS 629.
Mrajis Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Geita, Doreen Mwanri amesema kati ya vyama vyote 629 ni vyama 304 ndio vimesajiliwa kwenye mfumo unaovitambulisha kuwa ni vyama hai.
Amesema mpaka sasa kuna vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOSS) 18 pekee zilizokidhi sifa za kutambulika kama Vyama vya Ushirika na kujiendesha kupitia sheria ya huduma ndogo za fedha.
“Tumeanza kufanya tathimini ya namna gani fedha zinapotea bila kupitia benki ama simu, na katika taarifa yetu tutabainisha mdeni ambayo vyama vinadai lakini pia makampuni yanadai” amesema.



