ARUSHA: Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella ametoa miezi miwili kwa Mganga Mfadhiwi wa Kituo cha Afya Karatu Dk, Amani Mao kuhakikisha chumba cha kuhifadhia maiti kinafanya kazi tofauti na hivi sasa kugeuka stoo ya kuhifadhia vifaa chakavu.
Pia ameagiza stoo ya dawa iliyopo kituo hicho ihamishiwe Hospitali ya Wilaya ya Karatu kutokana na chumba hicho kuwa na giza huku uhifadhi wa dawa ukiwa haupo katika mpangilio.
Maagizo hayo yametolewa leo wilayani Karatu wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa huduma za afya sanjari na jengo la wodi ya kinamama na watoto ambalo limekaa muda mrefu bila kujengwa na kuleta nyufa katika kituo hicho.
Amesema haiwezekani chumba cha kuhifadhia maiti kikawa stoo huku majokofu nane ya kuhifadhia miili yakiwa hayafanyi kazi kutokana na hitilafu ya umeme unaokatika mara kwa mara na kupelekea miili mingine kuhifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Karatu.
“Hivi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dk, Charles Mkombachepa na timu yako ya afya huwa mnakuja kukagua nini katika ziara zenu serikali imewekeza zaidi ya Sh,bilioni 4 kujengwa hospitali ya Wilaya ya Karatu sasa hospitali ile inafanya kazi lakini wagonjwa wengi wanarundikana hapa sasa naagiza dawa zote zilizopo kituo hiki zipelekwe hospitali ya wilaya”
Lakini kwanini hapa mochwari imekuwa stoo na ndani yake kunavifaa tiba mnavyoweza kutengeneza na kwanini umeme unakatikatika hapa sababu ya jenereta hapa kuna uzembe fulani hivi lazima mjipange, lakini pia DMO Mkoa wasiliana na uongozi wa juu ulete Mganga Mkuu wa Wilaya na Mganga Mfadhiwi kwenye hospitali ya Wilaya ya Karatu ili huduma za afya zitolewe huko.
Naye Mganga Mfadhiwi wa Kituo cha Afya Karatu Dk,Mao alikiri chumba cha kuhifadhia maiti kutokufanya kazi kutokana mhandisi wa halamshauri ya wilaya hiyo kuchukua jenereta hilo na kulitengeneza kutokana na changamoto ya kuharibika kila wakati huku akikiri ni kweli kunaudhaifu katika sekta ya uhifadhi wa dawa za binadamu zinazohifadhiwa katika stoo hiyo.