REA yatoa majiko ya gesi 310 kwa maafisa magereza Geita

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imetoa majiko na mitungi ya gesi 310 yenye uzito wa kilo 15 kila moja kwa maofisa magereza mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi za umma.

Aidha REA imepanga kusambaza tani 19 za mkaa mbadala kwenye magereza manne ya mkoa wa Geita ambapo gereza la wilaya ya Geita litapatiwa tani 5, Chato tani 5, Kanegere tani 4 na Butundwe tani 5.

Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kutoka REA, Mhandisi Emanuel Yesaya ametoa taarifa hiyo Julai 04, 2025 katika hafla ya kuzindua mradi wa kusambaza nishati safi kwa watumishi wa magereza mkoani humo.

Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kutoka REA, Mhandisi Emanuel Yesaya.

Amesema watumishi wa gereza la wilaya ya Geita watapata mitungi 97, Kanegere mitungi 55, Chato mitungi 67, Butundwe mitungi 52, huku maofisa magereza makao makuu Geita wakipatiwa mitungi 40.

Amesema mradi huo unahusisha ufungaji wa miundombinu ya gesi asilia, bayogesi ipatayo 126 na LPG katika magereza 64, usambazaji wa mkaa mbadala tani 850 na ununuzi wa mashine 61 za kuzalisha mkaa mbadala.

“Katika mkoa huu gereza la Chato litanufaika na kufungwa mfumo wa LPG, na katika mashine za kutengeneza mkaa mbadala magereza ambayo yatanufaika mkoani hapa ni gereza la Kanegere”, amesema.

Amesema pia gereza la Geita litafungwa mfumo wa biyogesi pamoja na majiko matatu, chato mfumo mmoja na majiko mawili, Kanegere mfumo mmoja na majiko mawili na Butundwe mfumo mmoja na majiko matatu.

Mjumbe wa Bodi ya REA, Lucas Malunde.

Mjumbe wa Bodi ya REA, Lucas Malunde amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mkataba wa Septemba 15, 2024 uliosaniwa kati ya REA na Jeshi la Magereza kusambaza nishati safi ya kupikia kwenye magereza 129 nchi nzima.

Malunde amewaomba watumishi wa magereza kuendelea kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika jamii ili kulinda mazingira na kuokoa afya.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Magereza, Jonam Mwakasagule.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Magereza, Jonam Mwakasagule ameipongeza serikali ya awamu ya sita kupitia REA kwa maono makubwa ya mradi huo ambao utaongeza utendaji wa watumishi wa magereza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button