Ridhiwani : Tudumishe amani ya nchi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, mshikamano na uwajibikaji ili kuimarisha maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa futari maalumu iliyoandaliwa na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwa wadau wake, Ridhiwani amesema  mwezi mtukufu wa Ramadhan ni kipindi muhimu kinachowakumbusha waumini wa dini ya Kiislamu kuwajibika, kufanya mema na kuimarisha mshikamano katika jamii.

Amewataka viongozi na watendaji wa Shirika la Bima Zanzibar kuendelea kuzingatia maadili ya kazi na kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma ili kuimarisha sekta ya bima ambayo ni muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.

“Katika mazingira ya sasa ya kiuchumi, kunahitajika taasisi imara na zenye uwajibikaji ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi. ZIC imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za bima, jambo linalostahili kupongezwa,” alisema Ridhiwani.

Ameongeza kuwa maendeleo ya uchumi hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani na mshikamano, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuendelea kuilinda na kuidumisha amani ya nchi. “Tunapaswa kutambua kuwa maendeleo ya taifa letu yanategemea umoja na mshikamano. Tukilinda amani yetu, tutaendelea kufurahia matunda ya maendeleo katika sekta mbalimbali,” alisema.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Bima za Kawaida wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Sabri Omar Ali, amesema shirika hilo litaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utoaji wa huduma za bima kwa wananchi ili kuhakikisha zinawafikia watu wengi zaidi nchini.

Sabri amesema hayo wakati akimkaribisha mgeni rasmi katika futari hiyo, akieleza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni ZIC imepanua wigo wa huduma zake ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za bima zitakazosaidia kulinda mali na maisha yao dhidi ya majanga mbalimbali. SOMA: Uanzishwaji wa bima kunufaisha wananchi Zanzibar

Amesema upanuzi huo umewezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma za bima, hatua inayochangia kuongeza uelewa wa umuhimu wa huduma hiyo katika kulinda uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha ushirikiano na amani ili kuimarisha mahusiano kati ya taasisi na wadau mbalimbali, hali itakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. “Mafanikio ya uchumi hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani. Amani ndiyo msingi wa maendeleo ya biashara na utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” alisema Sabri.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button