RIPOTI MAALUM

Bandari bubu zikidhibitiwa, fedha zipo za kutosha

SERIKALI imekuwa ikipoteza mapato kutokana na uwepo wa bandari bubu katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa Bahari ya Hindi na maziwa yakiwemo Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Mei 20, 2022 akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema utafiti uliofanyika nchini umebaini kuwa hadi kufikia Juni 2021 ulionesha kuwepo kwa bandari zisizo rasmi 693, kati ya hizo bandari 239 ziko katika mwambao wa bahari ya Hindi, bandari 329 katika Ziwa Victoria, bandari 108 katika Ziwa Tanganyika na bandari 17 katika Ziwa Nyasa.

Hata hivyo, ripoti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inaonesha Dar es Salam kuna bandari bubu zaidi ya 300, Mtwara 250 na Tanga kuna bandari bubu 250.

Uchunguzi uliofanywa na HabariLeo katika bandari ya Mbweni pekee licha ya kutokuwa na miundombinu muhimu ya kisasa, serikali inaingiza kati ya Sh milioni 400 hadi sh milioni 800 kwa mwezi kutokana na ushuru wa bidhaa mbalimbali zinazoingizwa katika bandari hiyo.

Kama bandari moja ya Mbweni kwa wastani inaingiza sh milioni 600 kwa miezi 12 itakuwa inaingiza Sh biloni 7.2.

Dar es Salaam kuna bandari bubu 300 zingedhibitiwa kikamilifu zingeweza kuingiza Sh trilioni 2.5

Fedha hizo Sh trilioni 2.5 ambazo serikali inapoteza kila mwaka katika bandari bubu pekee za Dar es Salaam, zingeweza kujenga hospitali 860 za kisasa zenye hadhi kama ya Hospitali ya Kata ya Mabwepande, ambayo serikali imejenga kwa gharama ya Sh bilioni 2.5, ikiwa na huduma za wagonjwa wa kutwa (OPD) na kulala (IPD), ikiwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 1200 kwa siku, 500 wa kutwa na 700 wa kulazwa.

Ina vitanda vya kulaza 224, vyumba vya upasuaji, maabara, vyumba vya vipimo kama X -Ray, CT- Scan, Ultra Sound, ECG nakadhalika.

Pia, ina eneo la huduma za dharura, eneo la tiba ya mazoezi, eneo la huduma za kinywa, masikio, koo na macho, eneo la kuhifadhi dawa na eneo la kuhifadhi maiti.

Kwa upande wa madarasa kiasi hicho cha Sh trilioni 2.5 kingeweza kujenga madarasa 107,500 katika shule 5,375 yenye mikondo 20 kwa gharama ya Sh milioni 20 kwa kila darasa moja, lenye madawati 50 kwa shule za sekondari na madawati 25 kwa shule za msingi.

BANDARI BUBU ZIMWI:

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo anakiri kuwa bandari bubu ni mfupa mgumu, ni Zimwi linalonyonya mapato ya serikali.

“Ni kweli Bandari bubu zipo nyingi kutokana na kuwa na ukanda wa bahari wa kilomita takribani 1400 kutoka Mtwara hadi Tanga, katika ukanda huo tuna bandari rasmi chache kama Mtwara, Lindi, Kilwa, tunayo Dar es Salaam, Bagamoyo lakini humo katikati kuna bandari nyingine bubu nyingi tu,” amesema Kayombo na kuongeza:

“Ukanda wa bahari ni mrefu tunafanya doria, lakini si rahisi kuwa kila mahali, hivyo tunawategemea sana raia wema wanaotupa taarifa hasa inategemea na usahihi wa taarifa hizo.”Anasema

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanashauri serikali kurasimisha bandari bubu zote zilizoota kama uyoga ili kudhibiti mapato.

Pia wanazishauri Mamlaka za juu zaidi kuitazama kwa macho yote Bandari ya Dar es Salaam, ambayo wamedai kuwa uendeshaji wake na kasi yake ya ukusanyaji mapato unatia shaka.

Kwa mujibu wa Rais Samia Saluhu Hassan, alisema hivi karibuni kuwa mwaka 2019/2020 makusanyo katika bandari ya Dar es Salaam yalikuwa Sh bilioni 901, mwaka 2020/2021 Sh bilioni 896 na mwaka 2021/2022 katika robo ya kwanza ya makusanyo ilikusanya Sh bilioni 980 hadi mwisho wa mwaka.

Bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ni shilingi triioni 41, kwa kauli ya Rais Samia Suluhu, maana yake anaitazama bandari moja tu ya Dar es Salaam kuwa inaweza kuchangia mpaka Sh tirilioni 20 kwa mwaka, ikiwa kutakuwa na usimamizi madhubuti.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya Uchumi wanasema, bandari ya Dar es Salaam ikisimamiwa vizuri, bandari bubu zikarasimishwa, sekta hiyo ya uchukuzi ina uwezo wa kuchangia bajeti yote ya nchi bila kutegemea wafadhili.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Dk William anasema bandari ya Dar es Salaam ni moja ya bandari ya kimkakati na kifaida zaidi, pengine kuliko bandari nyingi za ukanda wa Afrika Mashariki.

“Bandari za Mombasa, Tanga, Mtwara na zingine kama za Djibouti, Sudan na Mauritius, zilivyokaa na miundombinu yake, zinaipa nafasi bandari ya Dar es Saaam kufanya vizuri zaidi,” anasema Dk William, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Lakini uendeshaji wake na kasi yake ya ukusanyaji wa mapato unatia shaka jambo ambalo hata Rais Samia Suluhu Hassan ameliweka wazi hivi karibuni akisema: ‘‘Siridhishwi kabisa na kasi za bandari, siasa zilizoko, longolongo zilizoko, mabandari yanaendeshwa kwa kasi kubwa (duniani), na biashara zinakua kwa kasi kubwa kupitia bandari, sisi bado tunasuasua,”alisema Rais Samia.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, ambae ni mbobezi katika masuala ya uchumi, Willhem Ngasamiaku anasema serikali ingeangalia namna ya kurasimisha bandari bubu zote kama imeshindikana kudhibiti.

Anasema, kama bandari ya Mbweni ambayo haina miundombinu rafiki ikiwemo barabara ya kuingia bandarini ni mbovu lakini inakusanya kati ya Sh milioni 400 hadi Sh mil 800 sawa na wastani wa Sh milioni 600 kwa mwezi, bandari bubu 300 zingedhibitiwa serikali ingepata fedha nyingi ambazo zingeweza kusaidia katika kuboresha miundombinu.

” Ukiwa na bandari 200 unapata sh bilioni 1.2 kwa mwezi, ‘performance’ ya bandari ya Dar es Salaam pekee ina uwezo wa kukusanya sh bilioni 100 kwa mwezi,” anasema.

Amesema, bandari peke yake ina uwezo wa kuchangia bajeti ya serikali kwa asilimia 1.3 na kuifanya serikali kuacha utegemezi kutoka kwa wafadhili, misaada ya wahisani na sekta binafsi.

“Bandari ya Dar es Salaam haijafikia ‘maximum ya potential’ ya mapato,” amesema Ngasamiaku na kuishauri TRA kuimarisha kitengo chao cha ‘Tax investigation surveillance’, ambacho bado kina uwezo mdogo na kutaka kiongezewe nguvu.

Habari Zifananazo

Back to top button