WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umetoa siku 30 kwa taasisi na asasi 743 zijieleze kwa nini bodi za wadhamini wa taasisi hizo zisifutwe.
Rita imeleeza kuwa bodi hizo hazijatekeleza maelekezo ya kufanya marejeo ya katiba na kupeleka marejesho ya kila mwaka ya taasisi hizo kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Angela Anatory, wakala umefikia hatua hiyo kutekeleza takwa la kisheria.
“Hizo taasisi na asasi 743 ni orodha ya awali, uchambuzi wa taasisi zaidi unaendelea lengo ni kuhakikisha wadhamini wa taasisi zote wanatekeleza majukumu yao kikamilifu kwa mujibu wa sheria, katiba na maslahi mapana ya taifa,” alisema Anatory.
Alisema Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini Sura ya 318, toleo la 2002 kifungu 23(1) (d) kinatoa maelekezo ya taasisi zote nchini zilizosajiliwa na Rita kufanya marejeo kwa mujibu wa sheria hiyo.
Anatory alieleza kuwa bodi hizo zina jukumu la kuwasilisha marejesho kwa msimamizi mkuu wa wadhamini kila baada ya miezi 12 na kuwa kushindwa kutekeleza takwa hilo ni kwenda kinyume na sheria na hatua dhidi yao zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuta bodi husika.
Aidha, alieleza kuwa msimamizi mkuu wa wadhamini alitoa agizo la kutekelezwa ndani ya miezi sita kuanzia Julai mwaka jana na kuzitaka bodi zote za wadhamini zifanye marejeo na kuboresha katiba zao kwa lengo la kuweka ibara inayoainisha chombo cha juu cha taasisi husika kwa taasisi za kidini.
Pia bodi hizo zilitakiwa kuweka ibara inayoelezea namna ya utatuzi wa migogoro unavyofanywa kwenye taasisi husika na kuweka ibara ya muda au ukomo wa wadhamini kukaa madarakani.