RITA yatoa elimu Wiki ya Sheria Dar, Dom

RITA yatoa elimu Wiki ya Sheria Dar, Dom

KATIKA Wiki ya Sheria inayoendelea katika Jiji la Dodoma na Dar es Salaam Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), inaendelea kutoa elimu kwa Bodi za Wadhamini zilizosajiliwa na RITA kufanya marejeo ya Katiba zao pamoja na kupata maelekezo ya kina kuhusu jinsi ya kufanya huduma hiyo kwa njia ya kielektroniki.

Kwa Dar es Salaam Maonesho ya Wiki ya Sheria yanaendelea katika viwanja vya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na Dodoma yanaendelea Nyerere Square.

Akifafanua  zaidi kwa waandishi wa habari wakili wa Serikali Peter Mbogoro, amesema kuwa bodi za wadhamini zilizosajiliwa na RITA, zinatakiwa kufanya marejeo ya katiba zao kwa kufanya marekebisho, ili kuboresha maeneo kama kuweka ibara inayoainisha chombo cha juu cha taasisi husika (Supreme Authority) kwa taasisi za kidini.

Advertisement

Pia kuweka ibara inayoelezea namna ya utatuzi wa migogoro inapotokea ndani ya taasisi, kuweka ibara inayoonesha muda wa ukomo wa wadhamini kukaa madarakani, kuweka ibara inayoonesha sababu za mdhamini kuondoka madarakani, kuweka ibara inayoonesha idadi ya vikao vya wadhamini kwa mwaka na majukumu yake, ikiwa pamoja na wajumbe wanaopaswa  kuhudhuria vikao husika na akidi kwa vikao hivyo.

Amesema taasisi zilizosajiliwa Ofisi ya Msajili na Jumuiya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na zinapaswa kusajili Bodi za wadhamini RITA, lakini hazijafanya hivyo huku akitumia nafasi hiyo kuzitaka kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Pia amesema bodi za wadhamini wa taasisi za kidini ambazo hazikusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani  zinaelekezwa kufanya hivyo.

Wakili Mbogoro amesema pia wanatoa elimu kwa umma kuhusu huduma za wakala, ikiwemo ya kuandika na kuhifadhi wosia ikiwa ni jitihada za kupunguza na kuondoa migogoro katika jamii, masuala yahusuyo mirathi ikiwa ni moja ya majukumu ya RITA kwa kuteuliwa na mahakama, masuala ya ndoa na talaka na pia tunasajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa.

 

/* */