WATU bilioni 1.2 wamehusika moja kwa moja kuona, kutazama, kuangalia na kuifuatilia Tanzania kutokana na filamu ya Royal Tour huku hifadhi za taifa zikivunja rekodi kwa kupata jumla ya watalii 1,412,719 kwa kipindi cha miezi tisa, idadi ambayo haijawahi kuipata.
Aidha, kumekuwa na ongezeko la mapato ya utalii maradufu ambapo mapato ya jumla ya sekta yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.310.34 (sawa na Sh trilioni 3.01) mwaka 2021 hadi Dola za Marekani bilioni 2.527.77 (sawa la Sh trilioni 5.82). Filamu hiyo ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana kuelezea mafanikio ya mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwa filamu hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi ametaja mafanikio 10 ya filamu hiyo. Dk Abbasi alisema kumekuwa na mafuriko ya mafanikio katika Royal Tour.
“Mwaka mmoja uliopita tulizindua Royal Tour na Watanzania waliiona rasmi, wakati tunatangaza Royal Tour hatukudhani kama tungefikia hapa,” alisema na kuongeza kuwa taasisi zote kubwa duniani zilizoifanyia ulinganifu na alama Filamu ya Royal Tour zimeipa alama kubwa pengine kuliko Royal Tour nyingine nane.
Alisema kuwa Mtandao wa TripAdvisor: Mtandao namba moja duniani katika kutangaza utalii umeipa Royal tour alama 5/5; Mtandao wa Amazon Video; umetoa alama 4.5/5; na Mtandao wa IMDb; Mtandao namba tatu duniani baada ya Youtube na Netflix umeipa Royal Tour alama 8.8/10.
Alisema kuwa kwa mujibu wa ripoti ya waandaaji wa Royal Tour, filamu hiyo si tu imeshaoneshwa katika vituo zaidi ya 300 vya televisheni vilivyoko kwenye majimbo yote Marekani, lakini tofauti na Royal Tour nyingine zote, filamu ya Tanzania imetajwa kuwa namba moja kwa kutazamwa zaidi na vituo vingi vya televisheni kulazimika kuirudia na vinaendelea kuirudia.
“Kwa mujibu wa ripoti ya Kampuni ya Peter Greenberg Worldwide (PGW), kawaida kiwango cha kutazamwa filamu za Royal Tour katika majimbo inakooneshwa hufikia wastani wa asilimia 67, lakini Royal Tour ya Tanzania imefikisha wastani wa kihistoria wa asilimia 81,” alisema.
Dk Abbasi alisema pamoja na filamu hiyo kupata alama kubwa kutazamwa na wengi kupitia Royal Tour, watu zaidi ya bilioni moja mpaka sasa wameijua, kuisikia, kuiona au kuifuatilia Tanzania.
Alisema kuwa takribani watu milioni 600 waliijua, kuisikia, kuifuatilia Tanzania kupitia mahojiano na matukio mbalimbali ya kihabari ambayo Rais Samia aliyafanya kabla, wakati na baada ya uzinduzi wa Royal Tour Marekani na hapa nchini.
Dk Abbasi alisema kuwa takribani Wamarekani milioni 100 wameiona Royal Tour kupitia Stesheni ya PBS na milioni tano wametazama kupitia mitandao ya kijamii ya PGW na kuwa hiyo ni mpaka Aprili Mosi, mwaka huu kupitia mitandao ya Amazon na Apple TV+.
Alitaja faida nyingine ni kuongezeka kwa uwekezaji ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Biashara nchini (TIC), hamasa na mguso wa filamu ya Royal tour imeongeza idadi ya wawekezaji nchini ikiwemo uwekezaji wa jumla.
“Akiwa Marekani mwaka jana, Rais Samia wakati wa Royal Tour pia alishuhudia mikataba ya awali minane (miwili ikihusu sekta binafsi na sita ya kiserikali). “Mikataba hii uwekezaji wake utafikia thamani ya zaidi ya Sh trilioni 11.7.
Baadhi ya wawekezaji hao wameshafika nchini na kupewa ardhi kama kampuni ya Camdemi HB (Hotel Arumeru); kampuni ya Polo Properties imeshasajili mradi TIC na kampuni za Northern New Feed zimeshafika nchini na taratibu zinaendelea.
Pia Uwekezaji Mahususi Sekta ya Utalii, TIC imeshuhudia ongezeko la miradi ya uwekezaji wa kitalii ikiwemo kusajiliwa mradi mkubwa wa Dola za Marekani milioni 300 uitwao Tourism Adventure Park utakaokuwa na hoteli, maeneo ya utalii wa kiutamaduni na michezo.
“Hadi Machi, 2023, jumla ya miradi mikubwa 26 ya uwekezaji katika utalii imesajiliwa, ikilinganishwa na miradi 16 Machi 2020 (kabla ya Royal Tour),” alisema. Aidha, alisema hamasa ya Royal Tour pia imeongeza idadi ya watalii wa ndani na nje na aliongeza kuwa watalii kutoka nje wameongezeka kutoka 620,867 mwaka 2020 hadi 1,454,920 Desemba, 2022 sawa na ongezeka la asilimia 57.7 na kwa takwimu za mpaka Machi, 2023 inaonesha mwaka huu tutavunja rekodi ya Taifa kwa watalii kutoka nje, watalii wa ndani wameongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi 2,363,260 mwaka 2022.
Taasisi za utalii zaweka rekodi Alisema Tanapa kwa miezi tisa tu (Julai, 2022-Aprili, 2022) ilivunja rekodi kwa kupata jumla ya watalii 1,412,719, idadi ambayo hawajawahi kuipata tangu waanzishwe Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa miezi tisa tu kama Tanapa tayari wana watalii 638,950 na mapato ya Sh bilioni 146.33 ambayo hawajawahi kuyapata.
Watalii wanaotembelea maeneo ya misitu TFS na uwindaji na picha, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeongezeka kutoka 96,150 hadi 218,000 na 38,000 hadi 159,000 mtawalia kati ya mwaka 2021 na 2022.
Dk Abbasi alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la mapato ya utalii maradufu, mapato ya jumla ya sekta yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.310.34 (sawa na Sh trilioni 3.01) mwaka 2021 hadi Dola za Marekani bilioni 2.527.77 (sawa la Sh trilioni 5.82).
Tanapa na NCAA wamevunja rekodi ya mapato kama nitakavyoeleza punde, sekta inaingiza asilimia 25 ya fedha zote za kigeni. Alisema kumekuwa na mafuriko katika viwanja vya ndege ambapo Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro pekee kama sampuli: Ndege za kimataifa zimeongeza ruti Tanzania; miruko ya jumla ya ndege za kimataifa KIA iliongezeka kwa asilimia 28 kutoka miruko 6,115 Aprili 2021 hadi 7,850 Aprili, 2023; Qatar Air na KLM wameongeza miruko kwa siku; mashirika haya mawili yameongeza miruko kutoka tisa hadi 12 (ndege mbili kwa siku) na miruko mitano hadi sita mtawalia kutokana na kuongezeka abiria baada ya Royal Tour.
Ndege ya Eurowings Discover (Lufthansa Group) ilianza Juni 2022 kuja Tanzania mara mbili kwa wiki moja kwa moja kutoka Frankfurt, Ujerumani kuleta watalii wa Ujerumani na Ulaya kwa ujumla.
Alisema kuwa kupitia mafanikio haya Tanzania sasa imepata morali ya kwenda kimataifa zaidi kuitangaza Tanzania: Royal Tour sio mwisho ni mwanzo wa kuitangaza nchi kimataifa zaidi hivyo Kamati mwaka mmoja sasa, imepokea na inaendelea kuchambua “Royal Tours”.