DAR ES SALAAM: AHMAD Ally, anayejulikana pia kama @kakamussa, ni mpiga picha mashuhuri na rubani wa drone ambaye ameiletea heshima Tanzania kwa kushiriki katika utayarishaji wa filamu ya MUFASA ‘The Lion King’, iliyotayarishwa na studio za Disney za nchini Marekani.
Katika mahojiano maalum na Daily News Digital, Ahmad Ally alieleza safari yake ya kushiriki kwenye mradi huu mkubwa wa kimataifa na jinsi filamu hiyo ilivyoinufaisha Tanzania. Zaidi ya asilimia 70 ya mandhari iliyotumika kwenye filamu hiyo imechukuliwa kutoka maeneo halisi ya Tanzania, huku vivutio vya asili kama Ziwa Natron na mapango ya Isimila vikipewa nafasi kubwa katika filamu hiyo.

Ahmad Ally ameeleza kuwa nafasi yake katika mradi huo ilimpa fursa ya kutumia utaalamu wake wa upigaji picha na urubani wa drone kuonesha uzuri wa Tanzania ulimwenguni. Kupitia kazi yake, mandhari ya kuvutia ya Tanzania yaliwasilishwa kwa ubora wa hali ya juu, jambo ambalo linatarajiwa kuongeza mvuto wa utalii nchini.
“Ilikuwa safari ya kipekee kushiriki katika filamu hii. Tanzania ina vivutio vya kipekee, na kupitia kazi yangu, nimeweza kuhakikisha kuwa dunia inatambua uzuri wa nchi yetu. Hii ni fursa adhimu kwa sekta ya utalii na sanaa za kidigitali nchini,” amesema Ahmad Ally.
Filamu ya MUFASA si tu kwamba inatoa burudani kwa mashabiki wa The Lion King, bali pia inaipa Tanzania nafasi ya pekee kwenye ramani ya filamu duniani kama ilivyofanikiwa filamu ya The Tanzania Royal Tour.
Kwa mchango wa Ahmad Ally, tasnia ya filamu na teknolojia ya picha imeendelea kusonga mbele, na inaonesha kuwa vipaji vya Watanzania vinaweza kushindana kimataifa.
SOMA: Royal Tour yabamba, yaonwa na bil 1.2
Kwa mafanikio haya, Tanzania inazidi kuonekana kama kitovu cha uzalishaji wa filamu zenye mandhari ya asili, na filamu hii inatarajiwa kuhamasisha watayarishaji wa filamu zaidi kutumia vivutio vya Tanzania kwa uzalishaji wa kazi zao.