WATUMISHI na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jumuishi ya Ruhinda iliyopo Kata ya Nyaishozi Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera wameishukuru serikali kwa kuwafikishia huduma ya umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Licha ya kupata huduma hiyo pia wameomba kuwaboreshewa miundombinu ya nishati ya kupikia.
Ombi hilo limekuja mara baada ya Bodi ya Rea ikiongozwa na Mwenyekiti Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu kufanya ziara shuleni hapo kujionea maendeleo ya miradi ya Rea vitongojini inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali.
Mwalimu Katorogo amesema wanatamani kutumia nishati ambayo ni rafiki wa mazingira ili kuendana na Sera ya Serikali ya kutunza mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuendelea kuleta huduma za umeme huku vijijini ikiwemo shule yetu ambapo tumeweza kupata manufaa makubwa kama vile kuokoa zaidi ya Sh 430,000 kwa mwezi ambayo ilikuwa ikitumika kuchapisha mitihani ya majaribio kwa wanafunzi wetu na sasa tunatumia gharama isiyozidi Sh 100,000.
Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amesema kuwa suala hilo la matumizi ya nishati shuleni hapo litapata mwarobaini ili kuhakikisha wanatumia nishati safi hivyo likifikishwa kwenye bodi halitakwama kwa sababu wao wanaunga mkono kampeni ya Rais Samia ya kuhakikisha wanachama wote wanatumia nishati safi ya kupikia.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Mhandisi Hassan Saidy amesema pale palipo na giza panahitajika kuongezewa umeme hilo ni jukumu lao kuhakikisha linafanikiwa pia kwa suala la nishati ya kupikia katika shule hiyo wanaendelea kulifanyia tathmini kwa kuweka mifumo ya gesi safi.
Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka Rea, Jones Olotu amesema kuwa vitongoji 3,765 vya Mkoa wa Kagera vinatarajiwa kunufaika na nishati ya umeme wa Rea ambapo vitongoji 1887 kati ya hivyo tayali vimepata umeme kutokana na mpango wa serikali wa kuhakikisha umeme unafika kila kona.
Asifiwe Erasto ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza shuleni hapo amesema kupatikana kwa nishati ya umeme shuleni hapo imeongeza na kuimalisha usalama hususani kwa wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali ikwemo wenye uoni hafifi na wenye ualbino wakati wa usiku na wengine wanaweza kujisomea kutokana na uwepo wa mwanga wa kutosha.
Katika ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Rea kwenye Wilaya ya Karagwe pia walitembelea mradi wa maji uliounganishiwa huduma ya umeme na Rea kwa ajili ya kusukuma maji uliopo katika Kata ya Kituntu.