‘Rushwa ya ngono kikwazo wanawake kupanda uongozi’

MKURUGENZI Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa),  Rose Reuben amesema rushwa ya ngono ni moja ya visababishi vinavyochangia kuwanyima wanawake haki ya kupanda nafasi za juu za uongozi ndani ya vyumba vya habari.

Dk Rose ameyasema hayo, jijini Dar es Salaam, katika kikao cha majadiliano kilichoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T) kupitia mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari wanawake

Amesema, vitendo vya rushwa ya ngono waandishi wa habari wanawake wanaishia katika ngazi ya kuripoti tu habari, huku wachache wakipanda katika ngazi ya juu ya kuwa mwandishi mwandamizi, mhariri, mkurugenzi au meneja katika chombo cha habari.

Advertisement

Amesema kutokana na sababu hiyo Tamwa ilifanya utafiti mwaka jana uliothibitisha kuwapo kwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine wa kijinsia katika vyombo vya habari ukiwamo wa kimwili na maneno.

“Utafiti huu ulionesha kwamba zaidi ya asilimia 68 ya waandishi wa habari wanawake walikuwa wameathiriwa na vitendo hivi vya rushwa ya ngono, pia ulionesha wanawake hao hawakuwa tayari kuzungumza kwa sababu hawaoni msaada mbele yao huku wengine waliona kwamba ni aibu kuzungumza masuala hayo.

“Wengine hawakuwa tayari kuzungumza kwa sababu walikuwa wanalinda kazi zao, hivyo wanapambana hivyo hivyo kimjini mjini ili mradi aendelee na kazi yake, lakini wapo ambao walifukuzwa kazi na wengine waliamua kuacha kazi kutokana na kukataa kufanyiwa vitendo vya rushwa ya ngono,” amesema Dk Rose.

Amesema, katika kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo wamekuwa wakifanya mijadala mbalimbali na waandishi wa habari, ili waweza kufahamu kuwa hilo ni kosa la jinai, hivyo anapofanyiwa au kutengeneza mazingira ya kufanya hayo tayari anakuwa anakinzana na sheria na kuharibu tasnia ya habari.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *