Saba kizimbani kwa tuhuma za kuua kwa imani za kishirikina

WATU saba mkoani Singida wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuua mwanaume mmoja kisha kuchukua baadhi ya viungo vyake kutokana na kile kinachodhaniwa ni imani za kishirikina.

Waliofikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyoni mjini hapa ni pamoja na Othman Khamisi (50), Shaban Mussa (23), Mussa Swedi (60), Omary Jumanne (29), Salum Ibrahim (33), Oscar Issa (26) na Hamim Yahaya (24), wote wakazi wa Wilaya ya Manyoni.

Mwendesha mashitaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Ryoba Mkambala alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Felician Kapama kuwa Machi 3, mwaka huu, washitakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanaume mmoja ambaye jina lake halijafahamika hadi sasa, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 na 45 huku wakijua wazi kuwa hilo ni kosa kisheria.

Mkambala aliendelea kudai kuwa baada ya washitakiwa hao kumuua mwanaume huyo, walikata sehemu zake za siri pamoja na nywele zake, kucha na ulimi kisha kuondoka navyo kusikojulikana.

Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo, kitendo hicho ni kinyume na vifungu 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya adhabu Sura ya 16.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi za aina hiyo.

Mkambala aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuomba iahirishwe, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama hiyo na kupangwa Aprili 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.

Habari Zifananazo

Back to top button