Sababu saba TRA ikikusanya tril 32/-

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka rekodi kwa ukusanyaji wa mapato kwa kukusanya Sh trilioni 32.29 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Akizungumza kwenye hafla ya kupongezana na watumishi wa mamlaka hiyo na baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema mapato hayo yamevunja rekodi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996/97.
“Katika robo hii ya nne iliyoanza Aprili mpaka Juni ilipaswa kukusanya Shilingi trilioni 7.84 lakini mpaka Juni 30 ambayo ndiyo siku ya mwisho katika mwaka wa fedha, tumekusanya Shilingi trilioni 8.22. Na baada ya makusanyo hayo ya mwisho tumeweka rekodi ya kukusanya Shilingi trilioni 32.29 kwa mwaka wa fedha kote Tanzania Bara na Visiwani,” alieleza Mwenda.
“Awali lengo ilikuwa kukusanya Shilingi trilioni 31.65 lakini sasa tumevuka lengo kwa asilimia 16.7, ufanisi ni mkubwa kwa asilimia 103, ni mafanikio makubwa haya, rekodi ni kubwa tangu kuanzishwa kwa TRA,” aliongeza Mwenda.
Alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji kwa vitendo wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine, wafanyabiashara na watumishi ambao wanafanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa.
“Kipekee Rais (Samia) amekuwa na sisi kwenye kila hatua, lakini pia kitendo cha kushiriki Tuzo ya Walipakodi imekuwa hamasa kubwa kwa wafanyabiashara na hakuishia hapo, ameichukua kabisa na sasa itakuwa Tuzo ya Rais. Tunampongeza kwa hilo limezidisha hamasa kwa walipakodi,” alieleza Mwenda.
“Kingine alichotufanyia ni kuunda tume ambayo kazi yake kubwa ni kuangalia na kuboresha mfumo wa kodi, haya ni mapenzi makubwa, kipekee ametuwezesha kuajiri watumishi wapya 1,896, haijawahi kutokea TRA kuajiri watumishi wengi kwa mkupuo, ni sababu ya upendo wa Rais. Ndoto yetu ni mlipakodi afikiwe kwa haraka na tusiwe tena na madeni ya miaka mitatu, na hilo ndilo linalofanyika,” alibainisha.
Alisema sababu nyingine ya kupaa kwa mapato ni kuimarika kwa shughuli za kiuchumi.
“Lazima tukiri kuna ongezeko kubwa la mizigo bandarini, imezidi kuongeza mapato, lakini pia tumepunguza urasimu watoa huduma wako wengi huduma zinakwenda vizuri,” alisema bosi huyo wa TRA.
Alisema sababu nyingine ya mafanikio hayo ni kuimarika kwa ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara kwani kwa sasa wanakusanya kodi pamoja na wafanyabiashara wanafurahia mafanikio yao.
“Sasa hivi wafanyabiashara wanashiriki kutupa taarifa kina nani wanatukwamisha tusifikie malengo, ushirikiano huo ndio umetufikisha hapa… nataka niwahakikishie tunapoanza mwaka mpya tutaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wote ndani ya nchi hii, pia tutaendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara kwa wakati, tutaendelea kusimamia usawa wa ulipaji kodi nchini kwa kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa,” aliahidi Mwenda.
Alisema TRA ilipoanzishwa ilipewa lengo la kukusanya Sh bilioni 539 kwa mwaka mikoa yote na walifanikiwa kukusanya Sh bilioni 531. “Leo hayo ni makusanyo ya baadhi ya mikoa na kuna wastani ukiangalia makusanyo yamepanda sana, tuna kila sababu kuona tumeweka rekodi ya kukusanya miezi yote 12 na kuvuka lengo,” alieleza.
Alisema juhudi zinazofanywa na watumishi na walipakodi zimefanya wastani wa makusanyo kupanda kutoka Sh bilioni 44 kwa mwezi TRA ilipoanza mwaka 1996 mpaka Sh trilioni 2.7 kwa mwezi.
“Inawezekana uchumi umekua, ufanisi umeongezeka lakini lazima tukiri na ufanisi wa TRA umeongezeka kwa kiasi kikubwa sana,” alieleza Mwenda.