Sabaya kortini leo peke yake

Sabaya kortini leo peke yake

KESI ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2022 inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya inatarajiwa kutajwa leo.

Sabaya ni mshitakiwa pekee katika kesi hiyo baada ya waliokuwa washtakiwa wenzake wanne kukiri kosa na kutiwa hatiani kwa makosa mawili wiki iliyopita.

Washitakiwa hao ni Silivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.

Advertisement

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salome Mshasha, Mkurugenzi Msaidizi wa Kurugenzi ya Mashtaka, Maternus Marandu alidai washtakiwa waliandika barua ya kukiri kosa.

Alidai washitakiwa kwa pamoja walikubali kufanya makubaliano kwa mujibu wa sheria ili kufutiwa mashitaka yanayowakabili.

Walisomewa mashitaka mawili mapya ya kujitwalia mamlaka ya kufanya upekuzi nyumbani kwa mfanyabiashara Alex Swai na kula njama kushinda utaratibu wa haki.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi iliwatia hatiani washitakiwa hao na kuwataka kulipa faini ya Sh 50,000 kila mmoja kwa kila kosa katika mashitaka mawili waliyokiri.

Aidha washtakiwa hao pia walitakiwa kulipa fidia ya Sh mil moja kila mmoja kwa mwathirika wa tukio hilo, Godbless Swai mkazi wa wilayani Hai.

Katika kesi ya msingi, upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Ole Sabaya uliomba shauri hilo lihamishiwe Mahakama Kuu ili kesi hiyo ianze kusikilizwa na mshtakiwa aelewe hatma yake.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome, wakili wa utetezi, Hellen Mahuna alisema kuhamishwa kwa maelezo, vielelezo, ushahidi na masuala mengine kutaipa Mahakama Kuu uwezo kuendeleza shauri hilo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.