Safari treni ya Tazara kurejea Februari 10

SHIRIKA la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) limetangaza kurejea kwa safari za treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda New Kapiri Mposhi nchini Zambia kuanzia Februari 10, mwaka huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa maboresho na marekebisho mbalimbali ya kiufundi na kiutendaji yaliyolenga kuboresha huduma za treni za abiria zinazovuka mipaka kati ya Tanzania na Zambia.
Safari hizo zilikuwa zimesitishwa tangu Juni 2024 kutokana na changamoto mbalimbali.
SOMA: Bil 13/- zatengwa kuboresha Tazara
Katika taarifa iliyotolewa na shirika hilo, ilieleza kuwa changamoto zilizosababisha kusitishwa kwa safari hizo zimeendelea kufanyiwa kazi, hali iliyowezesha kurejeshwa kwa huduma hiyo muhimu ya usafiri wa kikanda.
Taarifa hiyo ilisema kurejea kwa safari za treni kutaimarisha dhamira ya msingi ya shirika hilo ya kukuza usafiri wa kikanda, biashara, utalii pamoja na kuimarisha mahusiano ya kijamii kati ya wananchi wa Tanzania na Zambia.
Kwa mujibu wa maboresho yaliyofanyika, safari rasmi za treni za abiria kati ya Dar es Salaam na New Kapiri Mposhi zitazinduliwa Februari 10, mwaka huu katika Kituo cha New Kapiri Mposhi.
Aidha, idadi ya safari za treni hiyo imepunguzwa kutoka nne kwa wiki hadi mbili, hatua inayolenga kuimarisha matumizi bora ya mabehewa na injini za treni.
Chini ya maboresho hayo mapya, treni kutoka Dar es Salaam kwenda New Kapiri Mposhi itaondoka kila Ijumaa saa 9:50 alasiri, huku safari ya kutoka New Kapiri Mposhi kwenda Dar es Salaam ikifanyika kila Jumanne na treni itaondoka saa 8:00 mchana kwa saa za Afrika ya Kati.
Sambamba na hilo, treni hiyo itatoa huduma za safari za haraka na za kawaida na katika safari za haraka, treni itasimama katika vituo vikubwa pekee ambavyo ni New Kapiri Mposhi, Kasama, Nakonde na Msolwa, huku treni ya kawaida ikisimama katika vituo vyote vilivyopo njiani.
Katika maboresho hayo pia, treni hiyo itafanya safari fupi za kawaida kati ya Udzungwa mara mbili kwa wiki na kati ya Kidatu na Makambako nchini Tanzania kwa lengo la kukidhi mahitaji ya huduma hiyo kwa wateja wa mikoa ya Morogoro na Njombe.
Tazara imeeleza kuwa maboresho hayo yamefanyika kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na lengo la kuboresha ufanisi wa huduma za usafiri wa reli katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.



