Safari za ndege Mtwara zarejea

SHIRIKA la Ndege la Air Tanzania (ATCL) limeanzisha tena safari zake katika Mkoani Mtwara baada ya kusitishwa kwa muda sasa.
Akizunguza mkoani Mtwara wakati wa uzinduzi wa safari za ndege za shirika hilo la ATCL, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Arif Jihann amesema Mtwara inanafasi muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na rasilimali zilizopo.

Amesema kurejeshwa kwa safari hizo kutachochea ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo uwepo wa nishati ya gesi ,uvuvi , kilimo biashara na utaliii wa fukwe.
Meneja wa Uwanja wa Ndege Mkoa wa Mtwara, Jordan Mchami amesema kutokana na kuwepo kwa gharama ndogo za nauli kwenda na kurudi kutoka mtwara kwenda Dar es Salaam ni Sh 199,000 kutapelekea kuongezeka kwa abiria watakaotumia usafiri huo.
“Hapo awali tulipokuwa na shirika moja la ndege nauli ilikuwa Sh 300,000 hadi Sh 400,000 mpaka Sh 500,000 mana yake ni hakukuwa na ushindani,” amesema Mchami.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya amesema uamuzi wa kurejeshwa kwa safari hizo sio tu zitafungua milango mipya kwa Mtwara kama kitovu muhimu cha biashara, uwekezaji na utalii lakini zitatatua changamoto kubwa za usafiri wa anga ambazo wakazi wa mtwara na mikoa jirani wamekuwa wakizikabili kwa muda mrefu .
“Kurejea kwa air Tanzania hapa Mtwara kumerahisisha urahisi wa safari na mumeweka nauli punguzo maalum la Sh 199,000 kwa safari ya kwenda na kurudi “amesema mwaipaya
Kwa Upande wao baadhi ya wananchi wanaotumia usafiri huo akiwemo Asina Nanyanga amesema ujio wa ndege hiyo Mtwara imekuwa ni fursa kubwa kwao kwasababu itarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi zaidi.



