Safari za usiku zapunguza vurugu msimu wa sikukuu

Na Waandishi Wetu

UPATIKANAJI wa usafiri wa mabasi kuelekea mikoa mbalimbali nchini saa 24 nyakati za asubuhi, mchana na usiku kumetajwa kuwa chanzo cha kupungua kwa adha ya usafiri kuelekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka.

Walisema pia ukataji wa tiketi mtandaoni umechangia kutopanda kwa nauli huku wengine wakidai kuwa upandishaji wa nauli hutokana na tamaa za wamiliki wa vyombo vya usafiri.

Advertisement

Mohamed Juma alilieleza HabariLEO kuwa matumizi ya tiketi za mtandaoni na kuwepo kwa usafiri kwa saa asubuhi, mchana na usiku imerahisisha upatikanaji wa usafiri huo.

“Msimu huu nauli zimebaki palepale bado tunatumia nauli zilezile za mwaka jana. Lakini watakaoamua kupandisha nauli, wachukuliwe hatua,’’ alisisitiza.

Naye, Mwanaisha Salum alisema kuwa miaka iliyopita kulikuwa na shida ya usafiri pamoja na kupanda kwa nauli kutokana na idadi kubwa ya wasafiri, lakini kwa mwaka huu hali imekuwa tofauti.

“Nimesafiri usiku kwa basi kutoka Dar es Salaam kuja hapa Mbeya, kwenye basi kulikuwa na nafasi saba hazina watu, pia nauli ni ile ile ya Latra, nimeshangaa sana kwani sijazoea kuona hali hii mwishoni mwa mwaka. Nadhani hali ya uchumi imechangia watu wengi kutosafiri mwaka huu,” alisema Salum.

Abiria mwingine, Musa Mbaga alisema hatua ya mabasi kusafiri saa 24 imesaidia kupunguza msongamano wa abiria ambao ulikuwa ukiendelea hasa mwishoni mwa mwaka kwamba sasa abiria wanasafiri asubuhi, mchana na usiku, hivyo kupunguza adha ya usafiri iliyokuwepo hapo awali.

Kwa upande wake, Seleman Mfanga alisema watoa huduma za mabasi wamejiwekea utaratibu wa kujipatia kipato wakati huu watoto wanapofunga shule wanapandisha nauli na wakati mwingine wanakosa magari.

Alisema magari kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro yamekuwa changamoto kupata na nauli imepanda.

Wakazi wa jijini Arusha, John Sanweli na Loela Lucas waliiomba serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha wanasimamia bei halisi ya usafiri wa mabasi ya mikoani ili kuondoa sintofahamu kwa abiria wanaotumia usafiri huo kwamba baadhi ya wamiliki wa mabasi wamekuwa na tamaa ya kupandisha nauli kiholela.

Sanweli aliomba pia wamiliki wa mabasi kutoa tiketi za kieletroniki ili kuondoa ukwepaji wa kodi kwani baadhi yao wamekua wakidai kwa abiria mtandao unasumbua na kutoa tiketi za kawaida huku wakikwepa kodi.

Naye Kondakta wa basi la Kampuni ya Golden Deer, Ally Husein alikiri kuwa idadi ya abiria imekuwa ndogo tofauti na walivyozoea miaka iliyopita, alikubaliana na sababu ya mabasi kusafiri saa 24, akisema kuwa hatua hiyo imepunguza msongamano wa abiria uliokuwa ukijitokeza hasa mwishoni mwa mwaka.

Pia, Wakala wa Mabasi, Mrisho Said alisema kupanda kwa nauli kunatokana na haraka za abiria wanapotaka kusafiri.

Alisema abiria wanaweza kutoa gharama mara mbili ili kununua tiketi itakayomwezesha kusafiri licha ya kuwepo kwa kiwango husika.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wasafirishaji wa Abiria Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Manyara (AKIBOA), Adolf Locken alisema serikali haijatangaza kupanda kwa nauli hivyo atakayepandisha nauli hizo atakuwa amepandisha kwa maamuzi yake binafsi na si kauli ya serikali.

“Kwa umoja wetu haujapandisha nauli na tumejipanga mwaka huu kuhakikisha hakuna abiria atakayekosa usafiri kwenda kula sikukuu za mwisho wa mwaka,” alisema Locken.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Takwimu za Makosa Barabarani, Mwanshamba Onesmo alisema wanaendelea kuchukua hatua kwa madereva wanaokiuka sheria na kuwataka wamiliki kutopandisha nauli kipindi hiki na badala yake zibaki kama zilivyo.

“Tunakemea kuzidisha abiria kwenye magari au kuchanganya abiria na mizigo, tutafanya operesheni zetu tukiwabaini tutawachukulia hatua,’’ alisema Onesmo.

Imeandaliwa na Veronica Mheta, Shukuru Mgoba na Francisca Emmanuel.