Samia aagiza wahitimu Veta wasaidiwe kujitegemea  

RAIS Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha unatenga asilimia 10 ya fedha za halmashauri zinunue vifaa na kuwatengea maeneo vijana watakaohitimu katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha mkoa huo (Kagera RVTSC).

Alisema jambo hilo ni muhimu ili kuwezesha vijana kutumia ujuzi kujiajiri na kusaidia taifa badala ya kuwa na kundi la waliohitimu Veta na kuwa tegemezi.

Rais Samia alisema hayo jana wakati wa makabidhiano ya chuo hicho kilichopo eneo la Muhongere, Kijiji cha Burugo, Kata ya Nyakato, Bukoba mkoani Kagera.

Alisema mkoa unapaswa ujipange ili kufahamu vijana watakaomaliza chuoni hapo wawanunulie vifaa vitakavyowasaidia kujiajiri na kuajiri wengine.

”Pamoja na serikali kutumia Sh bilioni 1.1 kuendesha chuo hiki kila mwezi, naahidi kuwalipia vijana 20, wanawake 10 na wanaume 10 kati ya 400 ambao hawana uwezo kabisa wa kujilipia. Lakini pia naamini wazazi hamuwezi kukosa shilingi laki mbili ya kuwalipia watoto wenu kupata mafunzo baada ya kuvuna kahawa au biashara nyingine,” alisema Rais Samia.

Alisema chuo hicho kina manufaa katika kupambana na maadui wakubwa watatu ambao ni ujinga, umasikini na maradhi na kwamba kinaongeza thamani kwenye elimu wanayoitoa katika kuongeza ujuzi.

Rais Samia alisema nchi itaendelea kuweka na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwa na uchumi unaoendeshwa na viwanda kwani zipo kampuni na viwanda vingi nchini zinazohitaji vijana wenye ujuzi.

”Tunahitaji vijana mafundi stadi katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo wa bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanzania, usambazaji wa umeme vijijini na shughuli nyingine za kitaifa na halmashauri ambazo vijana watahitajika ili miradi hiyo iende vizuri,” alisisitiza.

Raia Samia alisema utafiti uliofanywa na Idara ya Takwimu mwaka 2021 unaonesha asilimia 12 ya vijana wote nchini hawana ajira. Alisema serikali itahakikisha inajenga Veta katika wilaya zote ili kuwajengea uwezo wa kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.

Alisema wataendelea kutenga Sh bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo hadi wilaya zote 139 zitakapokamilika kwani bado wilaya 62 zisizokuwa na vyuo hivyo pamoja na Mkoa wa Songwe.

Vilevile, aliwataka vijana mkoani Kagera kutumia fursa ya chuo hicho kujiendeleza na mafunzo ya kuongeza ujuzi ili waweze kuchangia maendeleo yao binafsi na uchumi wa taifa.

”Wanapohitimu wataweza kupata ajira kwa urahisi katika kampuni nyingi nchini, kujiajiri kwa kuanzisha karakana zao zitakazowasaidia kuendesha maisha yao na kuajiri wengine,” alieleza.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema ujenzi wa chuo hicho umegharimu Sh bilioni 22. Alisema kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 400 wa kozi za muda mrefu na wanafunzi 1,000 wa kozi za muda mfupi. Pia kitatoa huduma ya malazi kwa wanafunzi 320.

Alisema utekelezaji wa mradi huo umehusisha majengo na miundombinu ambayo matatu ni ya karakana za mafunzo, madarasa, ukumbi wa mihadhara, maabara ya kompyuta na chumba cha maktaba, jengo la ofisi za walimu, jengo la utawala linalojumuisha ofisi.

Habari Zifananazo

Back to top button