Samia aahidi uchumi imara Singida

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema wananchi wakimchagua serikali ya chama hicho itatekeleza miradi itakayofungua biashara na uchumi wa Mkoa wa Singida.

Samia ametoa ahadi hiyo katika mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Bombadia, mjini Singida.

Amesema kuanzia mwaka 2021 mkoa huo ulipokea takribani Sh trilioni 1.7 kwa ajili ya maendeleo hivyo akichaguliwa serikali ya CCM itakamilisha miradi iliyoanza na kuanzisha mingine itakayoifungua Singida kibiashara na kiuchumi.

Samia ametaja baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa soko la kimataifa la vitunguu na ujenzi wa Soko la Machinga Complex.

Pia, amesema akichaguliwa ataanzisha kongani ya viwanda mkoani humo ili kuongeza fursa za ajira na kuongeza thamani kwa mazao yanayozalishwa Singida.

SOMA: CCM yaahidi kufanya makubwa

“Pia, kwa kuwa tuna uwanja wa ndege mkubwa wa Msalato (Dodoma) na SGR, lakini tukijaliwa tutajenga uwanja wa ndege ndani ya Singida na hizo ni fursa za kuifungua Singida kibiashara,” amesema Samia.

Ameongeza: “Niwaombe sana wana Singida fursa hizi ninawapeni nafasi za kujipanga kibiashara tafadhali tumieni fursa hizo ili kujiinua kiuchumi.”

Akizungumzia miradi ya maendeleo katika mkoa huo, Samia amesema CCM iliahidi kufikisha umeme katika vijiji vyote 441 mkoani hapa kazi ambayo imekamilika.

Amesema serikali inaendelea kusambaza umeme katika vitongoji, kazi ambayo inatarajiwa kukamilishwa ndani ya miaka mitano ijayo.

Samia amesema serikali imeupelekea Mkoa wa Singida takribani Sh bilioni 81.1 kwa ajili ya kukarabati na kujenga upya skimu za umwagiliaji zilizonufaisha wakulima 12,167 kutoka vijiji 67 vya mkoa huo.

Masoko ya mazao
Samia amesema kwa mkoa huo mwaka jana ulianzishwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao kupitia soko la mtandao kwa mazao ya dengu, mbaazi, choroko na ufuta kwa maeneo yanayozalisha ufuta.

“Hatua hiyo ya kubadili mifumo imesaidia kuongeza uwazi, kwa mfano mwaka jana pekee wastani wa bei ya mkulima ilifika asilimia 70 ya bei ya soko la dunia ambayo alipata mkulima hapa Tanzania,” amesema.

Ameongeza: “Nafahamu zipo changamoto za wanunuzi kuchelewesha malipo badala ya kulipa ndani ya saa 48 wanachukua siku tatu hadi nne, lakini nataka niwaambie tayari serikali imekwishachukua hatua.”

Ametaja hatua hizo ni kuwafutia leseni wanaohujumu mfumo huo ikiwemo wanaoweka uchafu kwenye mazao na wanaonunua nje ya mfumo.

“Hawatapatiwa tena kibali cha kuuza nje yaani hao ndio wameshajiondoa kwenye soko, lakini hapa kuna ombi la mgombea ubunge wa Ilongelo (Haidary Gulamali) kwamba dengu zipo ghalani unatuambiaje?” amesema Samia.

Ameongeza: “Nataka kusema kwamba tunahangaika kutafuta masoko, wakulima wenye mazao tulieni, tutatoa vibali vya kusafirisha nje kwa wale ambao tutawapa vibali, lakini bado tunahangaika kutafuta soko la dengu
na mbaazi.”

Samia amesema serikali ipo katika mazungumzo na Serika li ya India kuwatafutia wakulima masoko. Amesema mazungumzo yamefikia pazuri na bei haitashuka chini ya soko la dunia.

“Pamoja na kuwa bei ya dunia imeshuka na bei ya mnadani ni bora zaidi kuliko ya madalali lakini niwahakikishie kuwa hatutashuka chini ya asilimia 60 ya bei ya soko la dunia,” amesema.

Samia amesema pia mfumo wa ushirika utapitiwa upya ili uwe wenye tija zaidi kwa mazao hayo na kusisitiza kuendelea kutoa ruzuku kwenye mbolea na pembejeo na kuanzisha vituo vya kukodisha zana za kilimo kwa bei nafuu.

Amesema uwekezaji unaofanyika nchi nzima ni kwa ajili ya kujali utu wa mtu. Aliwaomba Watanzania kuipa ridhaa CCM ikafanye makubwa zaidi yanayomjali Mtanzania.

“CCM inaweka ilani yake inayojikita katika uwekezaji kwa kutumia fedha nyingi kama zinavyotajwa ili kujali na kuinua utu wa mtu. Tunataka kila Mtanzania tujali utu wake. Tujali afya yake, tujali elimu yake, tujali usalama wake, tujali kila kitu kinachomgusa Mtanzania hata uchumi na ustawi wake,” amesema Samia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button