Samia ahimiza ushirikiano nchi maskini

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa mwito kwa nchi zinazoendelea kudumisha amani na kushirikiana ili zipate maendeleo. Kwa mujibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini China, Rais Samia ameyasema hayo alipohutubia katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa kimataifa wa ngazi ya juu kuzungumzia ajenda ya maendeleo uliofanyika jijini Beijing jana.

“Tunahitaji jitihada za pamoja kudumisha amani, maendeleo na ushirikiano. Tunahitaji kuelewa kwamba kujitenga na migogoro haviwezi kutuwezesha kupata matokeo chanya,” alisema Rais Samia.

Kupitia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa twitter, ubalozi huo ulieleza kuwa mkutano huo uliandaliwa na Serikali ya China na Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping alitoa salamu katika hafla ya ufunguzi.

Advertisement

Rais Samia aliishukuru Serikali ya China kwa kumualika azungumze kwenye mkutano huo. Alisema mkutano huo utaionesha dunia umuhimu wa kuzisaidia nchi zinazoendelea hasa barani Afrika zipate maendeleo kwa kuwa jambo hilo ni la kibinadamu.

Rais Samia alisema kwa miaka mingi nchi zinazoendelea zimekuwa zikifanya jitihada kuzikabili changamoto zipate maendeleo. Alihimiza umuhimu wa mataifa kushirikiana kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN).

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *