Samia aishukuru AfDB ujenzi miradi Tanzania
RAIS Samia Suluhu Hassan ameishukuru na kuipongeza Taasisi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuwa mdau mkubwa wa sekta ya miundombinu nchini ambapo wamewezesha mkopo wa Sh bilioni 630 kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbamba Bay kwa kiwango cha lami.
Samia ametoa pongezi hizo leo Septemba 25, wakati akizungumza na wananchi wilayani Nyasa mara baada ya kufungua barabara ya Mbinga – Mbamba Bay (km 16) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh bilioni 122.76 mkoani Ruvuma.
“Nataka niwaambie Benki ya AfDB hawajasaidia barabara hii peke yake, ni wadau wetu wa barabara nchi nzima na hivi tunavyozungumza wanatusaidia kujenga barabara ya mzunguko ya njia nne katika mji Mkuu wa Dodoma,” Rais Samia amesema.
Samia ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na bidhaa na amewataka wananchi kutumia uwepo wa barabara hiyo kuleta maendeleo katika Wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma.
SOMA: Tanzania, AfDB zaungana kutekeleza miradi ya nishati
Samia ametoa wito kwa watumiaji wa barabara hiyo hususani madereva kuwa waangalifu ili barabara idumu.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ambapo wamekamilisha kujenga kwa kiwango cha lami mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 2,384 ambayo ni sawa na asilimia 20 ya mtandao wote wa barabara unaosimamiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS).
Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS ipo katika hatua za kutafuta wakandarasi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa madaraja mawili ambayo ni daraja la Mkili lenye urefu wa mita 20 pamoja na daraja la Mitomoni lenye urefu wa mita 80 ambalo litaunganisha Wilaya ya Nyasa na Songea Vijijini.
Le Fonds vert pour le climat approuve $151 M en faveur du programme de résilience climatique de @AfDB_Group dans la Corne de l’Afrique, renforçant les efforts d’adaptation dans la région.
En savoir plus : https://t.co/6MGEaKSt4W #ActionClimatique #AfriqueRésiliente pic.twitter.com/jWnB4DeJRr
— African Development Bank Group (@AfDB_Group) September 25, 2024
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Patricia Laverley, ameleeza utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya urafiki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na benki hiyo na kusema kuwa kukamilika kwa barabara ya Mbinga – Mbamba Bay kutasaidia kupunguza muda wa safari, nauli pamoja na gharama za matengenezo.