RAIS Samia Suluhu Hassan ameushukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa kuipatia serikali Sh bilioni 455 za miradi ikiwamo ya uchumi wa buluu. Jana Rais Samia alimshuhudia Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Natu Mwamba na Balozi wa EU nchini, Manfredo Fanti wakisaini mikataba mitatu ya kifedha jijini Dodoma.
Katika hafla hiyo, Balozi Fanti alitangaza msaada wa Sh bilioni 140 kusaidia utekelezaji wa bajeti ya Serikali ya Tanzania.
Dk Mwamba alisema programu zitakazotekelezwa kwa fedha hizo ziliandaliwa mwaka jana zikiwamo za kuendeleza uchumi wa buluu, kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi, fedha za kujiendeleza na za kuimarisha ushirikiano wa EU na Tanzania.
Rais Samia alisema miradi itakayotekelezwa kwa fedha za mikataba hiyo zitaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Alisema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni sehemu ya matokeo ya ziara aliyoifanya Februari mwaka jana Brussels nchini Ubelgiji ambako alikutana na Rais wa kamisheni ya EU, Ursula von der Leyen. Rais Samia alisema fedha hizo zitatumika kubadili sera, kuendeleza sekta za uchumi wa buluu, jinsia, mazingira, kuendeleza sekta ya kidijiti na kuboresha barabara za vijijini kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Alisema kwa miaka mingi sasa EU imekuwa mshirika wa maendeleo wa Tanzania kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi na amemshukuru Ursula von der Leyen kwa uwezeshaji huo. Rais Samia alisema tangu kuanza kwa ushirikiano na EU hadi sasa Tanzania imepokea misaada na mikopo isiyo ya kibiashara takribani shilingi trilioni 5.9 kupitia Benki ya Uwekezaji Ulaya (EIB) na zimekuwa chachu ya maendeleo kwenye sekta nyingi.
“Napenda kuwahakikishia kwamba programu zilizopata fedha zitatekelezwa kwa weledi na ufanisi,” alisema. Thamani ya mikataba mitatu Dk Mwamba alisema mradi wa uchumi wa buluu una thamani ya Sh bilioni 279.20 zitakazowezesha kukabili mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya pwani za Tanzania Bara na Zanzibar.
Mradi mwingine unahusu kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za serikali na kuendeleza sekta binafsi wenye thamani ya Sh bilioni 160.79. Dk Mwamba na Balozi Fanti walisaini mkataba wa mradi wa kuimarisha ushirikiano kati ya EU na Tanzania ili kuongeza ufanisi katika kubuni miradi na kuisimamia kwa ufadhili wa umoja.
Mradi huo una thamani ya Sh bilioni 15.23. Alisema Juni mwaka 2020, EU na Tanzania zilianzisha aina mpya ya ushirikiano kati ya EU na Tanzania utakaotekelezwa kwa miaka saba kuanzia mwaka 2021/2027. Alisema aina hiyo ya ushirikiano unahusu maeneo matatu yakiwamo mazingira, rasilimaliwatu, ajira na utawala bora.