Samia apokea waliohama CUF, Chaumma, Chadema

LINDI : MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amepokea wanachama wapya kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA). Samia alipokea wanachama hao katika mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
“Waliyoyaeleza ni mazito sana. Hivyo, nawashukuru kwa maoni yao. Wameona waje kuungana nasi na nina imani wale wengine ambao bado wana roho za kukereketwa wakiwasikia watu kama hawa, roho zao zitakuwa zinapoa na Mungu anawapa utulivu wa moyo, ili wote tuungane na Tanzania yetu, twende nayo kwa salama, utulivu na amani ili wote tuwe wamoja,” alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Lindi, Salum Barwany alisema amehamia CCM kwa kuwa ilani ya chama hicho itaufungua Mkoa wa Lindi. Barwany aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania kupitia CUF. Alisema ameona arejee CCM baada ya kuzipitia ilani za vyama vyote na kujiridhisha ilani ya CCM inaweza kuwavusha wana Lindi. “Chama chochote cha siasa malengo yake makuu ni kushika dola. Katika kushika dola, unatembea na ilani uliyokabidhiwa na chama chako kukiombea kura kishike serikali
Tangu uhuru, hakuna ilani kama hii ambayo inakuja kuifungua Lindi lakini leo Rais Samia ameweza,” alisema Barwany. Alisema watu wa Lindi wana imani na Mradi wa Kuchakata Gesi (LNG), ambao kwenye ilani ya CCM upo. SOMA: CUF yahimiza kupiga kura Oktoba 29
“Mradi una miaka 12 tangu nikiwa mbunge, viongozi mbalimbali wa kiserikali, wabunge, madiwani, mashehe, maaskofu wamepelekwa nchi mbalimbali kuangalia manufaa ya gesi lakini mpaka leo hatujapata. Kwa uwepo wako Rais Samia. Nina imani Lindi itafunguka, tutakuwa wezi wa fadhila kama bado watu wa Lindi hatutakuunga mkono,” alisema Barwany.
Wengine waliohamia CCM ni Yusuf Tamba, aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Mchinga kupitia Chaumma na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Lindi, Rehema Muhema na aliyekuwa Afisa Habari wa chama hicho, Abdul Kambaya. “Nilikuwa nagombea Jimbo la Mchinga, nikajifanya nataka kushindana na mama (Salma Kikwete wa CCM) lakini nikaona hakuna haja, CCM inatosha kutokana na mpangilio mzuri wa ilani yake.
Mimi leo ni mtoto wenu, narudi CCM mnipokee,” alisema Tamba. Rehema amehamia CCM na mume wake. “Nimekuja CCM, naomba tumpigie kura Rais Samia ili tushirikiane nae kuwatumikia wananchi,” alisema Rehema.