RAIS Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi wa kimataifa takribani 500 wakiwamo kutoka falme mbalimbali waliohudhuria mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II aliyeitawala Uingereza kwa miaka 70.
Malkia Elizabeth II aliyefariki dunia Septemba 8, mwaka huu, alifanyiwa mazishi ya kitaifa ya kwanza nchini Uingereza tangu mwaka 1965 alipofariki dunia Waziri Mkuu wa wakati wa vita, Sir Winston Churchill.
Takribani wageni 2,000 kutoka nchi mbalimbali duniani walijumuika na familia hiyo ya kifalme ya Uingereza na wawakilishi kutoka mashirika ya kutoa misaada katika kumsindikiza malkia huyo katika safari yake ya mwisho.
Shughuli nzima ya mazishi hayo ilianza Jumatatu asubuhi na Ibada Kuu ilianza muda mfupi kabla ya saa 5:00 kwa saa za Afrika Mashariki katika Kanisa la Westminster lililopo katikati ya Jiji la London.
Ilifuatiwa na ibada ya kujitolea saa iliyofanyika saa 9:00 alasiri katika mji wa Windsor na huduma ya kibinafsi na familia ilifanyika saa 12:30 jioni.
Umati mkubwa ulikusanyika mapema katika viunga mbalimbali vilivyoandaliwa jeneza hilo kupita huku wengi wa watu wakiwa na huzuni na wengine wakilia.
Mwili huo ulibebwa na gari la mizinga ukisindikizwa na askari 142 wa Kikosi Maalumu cha Wanamaji huku askari wengine wakiwa wamejipanga barabarani na maeneo mengine ya karibu ambako mwili huo ulipita.
Wafalme na wana wa wafalme 16 waliohudhuria mazishi hayo pamoja na marais zaidi ya 50 kutoka nchi mbalimbali dunia wakiwamo marais 10 kutoka Afrika.
Baadhi ya marais wa Afrika waliohudhuria ni Rais Samia, Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Dk William Ruto (Kenya), Paul Kagame (Rwanda), Ali Bongo (Gabon), Nana Akufo-Addo (Ghana)na Macky Sall (Senegal).
Uingereza iliwaalika wakuu wa nchi au mwakilishi katika ngazi ya mabalozi kutoka nchi yoyote ambayo ina uhusiano kamili wa kidiplomasia nayo.
Mataifa ambayo hayajaalikwa yalijumuisha Syria na Venezuela kwa sababu Uingereza haina uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia. Nchi nyingine ambazo hazikualikwa ni Urusi, Belarus na Myanmar baada ya kuziwekea vikwazo vya kiuchumi nchi hizo.
Viongozi mbalimbali wa dini walishiriki katika ibada za kumuombea safari ya mwisho malkia huyo akiwamo Mkuu wa Kanisa la Westminster, David Hoyle.
Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby ndiye aliyeongoza ibada ya kumkabidhi malkia kwa Mungu.
Askofu Mkuu wa Westminster, Msimamizi wa Mkutano Mkuu wa Kanisa la Scotland na Msimamizi wa Makanisa Huru aliongoza maombi.
Pia, Waziri Mkuu Liz Truss na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Scotland walitoa masomo kutoka katika maandiko wakati wa ibada kuu.
Tukio hilo lililoshirikisha viongozi zaidi ya 500 wa kigeni, wahudumu 4,000 na mabilioni ya watu duniani kote linakuwa ni tukio kubwa zaidi na la kipekee katika karne ya 21.
Maziko ya Malkia Elizabeth II yalifanyika jana jioni katika kaburi la Kasri la Mfalme George Windsor.
Katika eneo hilo dogo, baba yake Malkia Elizabeth II, Mfalme George VI pamoja na mamake Elizabeth Bowe na dada yake Mareret wamezikwa hapo.
Malkia Elizabeth II alizaliwa akiitwa Elizabeth Alexander May Windsor, Aprili 26, 1926 na kutawazwa kuwa Malkia wa Uingereza Februari, 1952 baada ya kifo cha baba yake, Mfalme George VI.