Samia atoa maagizo maji, fidia Mkinga

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa wizara mbalimbali ili kuboresha maisha ya wananchi wa Wilaya ya Mkinga.

Rais Samia alitoa maagizo hayo wilayani Mkinga mkoani Tanga jana alipozungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa maji Mkinga Horohoro unaotarajiwa kuhudumia wananchi 57,334 kutoka katika vijiji 37.

Aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii na ofisi inayohusika na mazingira kushirikiana ili kutunza vyanzo vya maji vinavyochangia maji katika Mto Zigi unaotumika katika mradi huo.

“Si leo tunatoa maji baada ya miezi miwili miezi sita maji yamekauka, hapana tutunze vyanzo maji yapatikane kwa uendelevu wake. Kwa hiyo wale wanaosimamia mabonde na vyanzo mbalimbali Muheza hadi Mkinga hivyo vyanzo vitunzwe vizuri,” alisema Rais Samia.

Aliziagiza pia mamlaka kuhakikisha zinasimamia shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo yanayopakana na mradi ili zisilete athari katika vyanzo vya maji ili maji yaende kwa wananchi kama inavyotakiwa.

Rais Samia aliwaeleza wananchi wa Mkinga kuwa serikali imejidhatiti kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na kuwahakikishia kuwa kwa kuwa mradi umefikia asilimia 46 na ujenzi unaenda kwa kasi basi maji yatapatikana muda mfupi ujao.

“Nimtake Waziri wa Maji na wizara kwa ujumla wasimamie mradi huu kwa ukamilifu ili maji yapatikane mapema zaidi. Najua muda wa kumaliza mradi ni mwezi wa 10 lakini inawezekana kila kijiji mnapokamilisha muachie maji yaende kwa wananchi ili vijiji vipate maji wakati mradi unaendelea,” aliongeza.

Aliitaka wizara kutosubiri hadi mradi wote umalizike na ufunguzi ufanyike ndipo wananchi wapate maji na kuongeza.

“Kwa sababu nimetoka kuutazama mradi unavyokwenda na kijiji cha karibu ni Mtimbwa, watu hawa wanapoenda kula Siku Kuu ya Eid ikiwezekana wawe wamepata maji, kama haitawezekana basi isizidi miezi miwili hawa watu wawe wamepata maji,” alisema.

Pia, Rais Samia alielekeza wananchi 56 ambao walipisha ujenzi wa mradi wa barabara ya Tanga hadi Horohoro na hawakulipwa kifuta jasho Wizara ya Ujenzi iangalie namna ya kuwapa kifuta jasho kwa sababu wenzao walilipwa.

Rais Samia alisema kuwepo kwa miradi ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Mkinga kumeifungua wilaya hiyo kwa wilaya zingine pamoja na mikoa mbalimbali nje ya Tanga.

Alisema ndani ya wilaya hiyo serikali imejenga Hospitali ya Wilaya ya Mkinga sambamba na ujenzi wa zahanati 15 kwa lengo la kuimarisha afya za wananchi wa Mkinga na Tanga kwa ujumla.

“Lipo soko la madini limejengwa ndani ya Wilaya ya Mkinga na kuboresha minada ya mifugo. Kwa namna ya kipekee tumefanya maamuzi ya kuleta Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe hapa Mkinga. Mambo haya yote yanakwenda kuifungua Mkinga yanakwenda kuongeza hadhi ya Wilaya ya Mkinga,” alisema Rais Samia.

Alisema pia, ujenzi wa barabara ya Mabokweni – Maramba – Daluni – Umba hadi Same yenye urefu wa kilometa 278 itajengwa kwa awamu.

Alisema kipaumbele ni maeneo korofi hususani maeneo ya Maramba kisha ujenzi utaendelea kadiri fedha zitakavyopatikana kwa sababu mradi huo bado haujapatiwa ufadhili na lengo ni kuijenga kwa kiwango cha lami.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button