Samia atoa msaada waliojifungua watoto njiti

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa mama waliojifungua watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Maweni mkoani  Kigoma.

Mahitaji hayo yamekabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,  Angellah Kairuki kwa niaba ya Rais Samia, mara baada ya kuweka jiwe la Msingi Jengo la kutolea Huduma za Wagonjwa wa Dharura (EMD) na Wagonjwa wa uangalizi Maalum (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya  Maweni mkoani  Kigoma leo  Oktoba 18, 2022.

“Rais Samia amewashika mkono Mama waliojifungua watoto njiti kwa kutoa mashuka, blanketi, vitenge, sabuni, pampasi, mafuta ya nywele na mahaitaji mengine ikiwa ni pamoja na vyakula kama mchele na sukari,” amesema Kairuki.

Kwa upende wake, Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel, amesema serikali italeta vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti, ikiwa ni pamoja na mashine za kufua hewa ya oksijeni, mashine za kuzalisha hewa joto na mashine za kutunza watoto njiti.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni, Dk Stanley Binag,i amesema vifaa tiba na mahitaji hayo yatasaidia utoaji wa huduma bora kwa watoto njiti  waliopo na wanaoendelea kuzaliwa katika hospitali hiyo.

Akitoa shukrani zake, mama wa mtoto njiti,  Halima Matayo amemshukuru Rais Samia kwa kuboresha huduma za afya nchini, hasa wa wakina mama, na kwa kutoa zawadi ambazo zitawasaidia katika kuwahudumia na kuwalea watoto wao.

Habari Zifananazo

Back to top button