Samia azidi kuimarisha diplomasia ya uchumi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ni nchi inayotekeleza makubaliano kwa vitendo.

Alisema hayo alipofanya mikutano miwili ya ngazi ya juu ya mazungumzo ya pande mbili mwanzoni mwa Mkutano wa 13 wa Dunia wa Serikali (WGS), unaofanyika katika eneo la Madinat Jumeirah, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu ameeleza mazungumzo hayo yanaakisi mkakati wa Tanzania wa diplomasia ya kiuchumi inayolenga matokeo halisi, kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa ikiwemo Afrika, Karibiani, Asia na taasisi za kimataifa.

Machumu alieleza pia yameoanisha ushirikiano wa kimataifa na vipaumbele vya taifa ikiwemo Dira 2050, uwekezaji, mageuzi ya utalii na uthabiti wa kijamii na kuimarisha taswira ya Tanzania kama nchi tulivu, inayofanya mageuzi na mshirika wa kuaminika.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, kuendeleza diplomasia ya kiuchumi na kuoanisha ushirikiano wa kimataifa na vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania.

Wakati wa mkutano na Waziri Mkuu wa Antigua na Barbuda, Gaston Browne walijadili masuala yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Karibiani, hususani kupitia mfumo wa Jumuiya ya Madola.

Browne aliipongeza Tanzania kwa uongozi na uwazi katika kushughulikia changamoto za kiusalama baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Rais Samia alimweleza Waziri Mkuu kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali zikiwemo kuanzishwa kwa Tume ya Uchunguzi, mipango ya kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa na maandalizi ya marekebisho ya Katiba.

Viongozi hao walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika ujumuishaji wa Afrika na Karibiani kupitia mfumo wa Jumuiya ya Madola; Biashara, uwekezaji na utalii, ikiwemo ushirikiano wa kitaalamu wenye muundo maalumu.

Pia, walikubaliana muunganisho wa usafiri wa anga kwa kuimarisha safari zilizopo kati ya Afrika na Karibiani; ushirikiano wa kiusalama na uhamishaji wa teknolojia; elimu na rasilimali watu ikiwemo kuunga mkono Mpango wa Masomo wa Jumuiya ya Madola wa Julius Nyerere na mabadilishano ya kijamii na ushirikiano wa kitamaduni kati ya wananchi.

“Ushirikiano huu unaendeleza maslahi ya kimkakati ya Tanzania ya kupanua ushirikiano wa Kusini kwa Kusini zaidi ya washirika wa jadi, kuiweka Tanzania kama kiunganishi kati ya Afrika na Karibiani, kutumia majukwaa ya Jumuiya ya Madola katika uwekezaji, elimu na uhamaji, na kuimarisha imani ya kimataifa kuhusu utawala, uthabiti na mwelekeo wa mageuzi nchini,” alieleza Machumu.

Katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), Shaikha Al Nuwais, Rais Samia alithibitisha dhamira ya Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na shirika hilo.

Shaikha aliisifu Tanzania kama mojawapo ya nchi vinara wa utalii duniani na kumtaja Rais Samia kuwa chapa imara ya kimataifa ya Tanzania, akirejea athari chanya za filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ katika kuvutia watalii.

Aidha, alithibitisha utayari wa UN Tourism kuunga mkono azma ya Tanzania ya kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni nane na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika Pato la Taifa kutoka asilimia 17 hadi asilimia 24.

Rais Samia alisisitiza Tanzania itaendelea kushikamana na misingi ya amani, uwazi, ushirikiano na utekelezaji wa
ahadi, misingi inayoongoza ushiriki wa Tanzania katika WGS 2026 na baadaye.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button