Samia azindua makao makuu ya mahakama Dodoma

DODOMA: Rais Samia Suluhu Hassan leo Aprili 5, 2025, amezindua jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jengo hilo limeweka rekodi kuwa la sita kwa ukubwa duniani miongoni mwa majengo ya mahakama na la kwanza barani Afrika.

Jengo hilo lenye ghorofa tisa na ukubwa wa mita za mraba 63,244, limejengwa kwa asilimia 100 kwa fedha za ndani ambapo jumla ya Sh bilioni 129.7 zimetumika katika ujenzi wake.

Mbali na jengo hilo, Rais Samia pia amezindua miradi mingine miwili ya mahakama ikiwemo jengo la utumishi wa mahakama pamoja na nyumba 48 za makazi ya majaji – hatua inayolenga kuboresha ustawi wa watumishi wa chombo hicho cha haki.

Jengo hilo la Makao Makuu ya Mahakama linajumuisha matawi matatu makuu ya mahakama nchini – Mahakama ya Upeo, Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu – huku ofisi za utawala zikiwa zimejengwa katikati ya muundo huo wa kisasa.

Katika kuendana na mageuzi ya kiteknolojia, jengo hilo lina mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayojumuisha matumizi ya akili unde (AI), maroboti ya kuwaongoza wageni, pamoja na eneo maalum la kutua helikopta, likiwa limetengenezwa kwa kudumu kwa zaidi ya miaka 100.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button