Waziri Lukuvi amesema kwa kutumia 4R za Rais Samia ikiwemo Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga Upya Taifa (Rebuilding) atahakikisha uchaguzi wa Serikali za Mtaa unakuwa huru na wa haki.
“Nataka niwatoe hofu vyama vyote 19 kuwa kwenye uchaguzi ujao chini ya Rais Samia utakuwa huru na wa haki,” amesema Lukuvi.
Waziri Lukuvi amevitaka vyama vyote vitakavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kujiandaa kushindana kwa sera ili wananchi waamue.
Akizungumzia ziara yake hiyo, Waziri Lukuvi amesema ziara hiyo ni ya kujitambulisha mara baada ya kuteuliwa nafasi hiyo.
Amesema katika wizara yake anasimamia (Sera, Bunge na Uratibu) moja ya majukumu ni kuvisimamia vyama vya siasa hivyo atavitembelea vyama vyote 19.
Kwa upande wake, Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi pamoja na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamesema ziara hiyo itaongeza hamasa ya ushirikiano
Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo,Dorothy Semu amempongeza Waziri Lukuvi kwa kufanya ziara hiyo na kumuomba kuondoa hofu ya wananchi kuhusu kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba mwaka huu.