Samia, Mpango watoa pole familia aliyechanganya udongo wa Muungano

RAIS Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wametoa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha miongoni mwa vijana wa Kitanzania walioshiriki katika tukio la kuchanganya udongo wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1965.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis aliwasilisha salamu hizo nyumbani kwa marehemu, Sifael Mushi, Makongo Juu mkoani Dar es Salaam jana.
Sifael alifariki dunia Februari 20 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Khamis alisema viongozi hao wakuu wapo pamoja na familia ya marehemu na wanatoa pole kwa kumpoteza mtu muhimu katika taifa hili na kwamba ataendelea kukumbukwa na kusomwa katika historia.
Alisema Sifael ameliachia taifa historia kubwa kwa kuweka historia ya Muungano ambao hadi leo matunda yake yanaonekana.
“Leo hii tunaona Muungano wetu ulivyo imara na unaendelea kudumu na hata wananchi wa pande zote mbili wanashirikiana, wanavuka maji (bahari) kutoka upande mmoja kwenda mwingine yote ni kwasababu ya kazi kubwa aliyoifanya mama huyu,” alisema Khamis.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alisema kizazi cha sasa kina mengi ya kutafakari na kujifunza kutokana na maisha ya viongozi walioasisi Muungano.
Mtambule alisema Sifael ni mfano wa kuigwa kwa kazi ya uzalendo na utii aliyouonesha alipokuwa miongoni mwa Watanzania walioshiriki kuchanganya udongo wa Muungano.
Mwili wa Sifael umesafirishwa kupelekwa Machame wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro na unatarajiwa kuzikwa leo.
Sifael alikuwa ni miongoni mwa vijana wanne wa Kitanzania walioshiriki tukio la kuchanganga udongo wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar wakati wa sherehe za mwaka mmoja wa Muungano uliosasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964.
Wengine walioshiriki katika tukio hilo na wametangulia mbele ya haki ni Hassanieli Mrema aliyefariki dunia Mei 4, 2023 Khadija Abbas Rashid alifariki dunia Agosti 22, 2023 na Omar Hassan Mkele aliaga dunia Agosti 28, mwaka jana.



